Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Wapende Watu Wote
2 Kaka zangu na dada zangu, ninyi ni wenye imani katika Bwana wetu mtukufu Yesu Kristo. Kwa hiyo msiwachukulie baadhi ya watu kuwa wa maana zaidi kuliko wengine. 2 Tuchukulie mtu mmoja anakuja katika mkutano wenu akiwa amevaa pete ya dhahabu ama akiwa amevaa mavazi ya thamani, na mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa na machafu naye akaja ndani. 3 Na tuchukulie kuwa mnaonyesha kumjali zaidi yule mtu aliyevaa mavazi mazuri na kusema, “Wewe keti hapa katika kiti hiki kizuri.” Lakini unamwambia yule mtu maskini, “Wewe simama pale,” au, “Keti chini karibu na miguu yetu.” 4 Je, hiyo haioneshi kwamba mnafikiri miongoni mwenu kuwa baadhi ya watu ni bora kuliko wengine? Mmesimama kama mahakimu wenye maamuzi mabaya?
5 Sikilizeni kaka na dada zangu wapendwa! Mungu aliwachagua wale walio maskini machoni pa watu kuwa matajiri katika imani. Aliwachagua kuwa warithi wa Ufalme, ambao Mungu aliwaahidi wale wanaompenda? 6 Lakini ninyi mmewadhalilisha walio maskini! Na kwa nini mnawapa heshima kubwa watu walio matajiri? Hawa ndiyo wale ambao daima wanajaribu kuyadhibiti maisha yenu. Si ndiyo hao wanaowapeleka ninyi mahakamani? 7 Je, si ndiyo hao hao wanaolitukana Jina zuri la Bwana wenu?[a]
8 Kama kweli mnaitunza sheria ya ufalme inayopatikana katika Maandiko, “Mpende jirani yako[b] kama unavyojipenda mwenyewe,”(A) mtakuwa mnafanya vizuri. 9 Lakini kama mtakuwa mnaonyesha upendeleo, mtakuwa mnafanya dhambi na mtahukumiwa kuwa na hatia kama wavunja sheria.
10 Ninasema hivi kwa sababu yeyote anayeitunza Sheria yote, lakini akaikosea hata mmoja tu atakuwa na hatia ya kuihalifu Sheria yote.
11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,”(A) pia ndiye aliyesema, “Usiue.”(B) Hivyo, kama hutazini lakini ukaua utakuwa umevunja Sheria yote ya Mungu.
12 Mseme na kutenda kama watu watakaokuja kuhukumiwa kwa sheria inayoleta uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu ya Mungu haitakuwa na huruma kwake yeye ambaye hakuwa na rehema. Lakini rehema huishinda hukumu!
Imani na Kazi Njema
14 Ndugu zangu, ikiwa mtu atasema kuwa anayo imani lakini hafanyi kitu, imani hiyo haina manufaa yoyote. Imani ya jinsi hiyo haiwezi kumwokoa mtu yeyote. 15 Kama ndugu au dada anahitaji mavazi na anapungukiwa chakula cha kila siku, 16 na ukawaambia, “Mungu awe nanyi! Mkahifadhiwe mahala pa joto na mle vizuri!” Hiyo ina manufaa gani kwao? Usipowapa vitu wanavyovihitaji, maneno yako yanakosa maana! 17 Kwa jinsi hiyo hiyo, imani isipokuwa na matendo itakuwa imekufa.
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mt 15:21-28)
24 Yesu akaondoka mahali pale na kuenda katika eneo lililozunguka Tiro. Aliingia katika nyumba na hakutaka mu yeyote ajue hilo, lakini hakuweza kufanya siri kuwepo kwake. 25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo mchafu mara moja akasikia juu ya Yesu hivyo alimwijia na kuanguka chini yake. 26 Mwanamke huyo alikuwa ni Mgiriki na siyo Myahudi, na alikuwa amezaliwa Foeniki ya Shamu. Yeye alimsihi amfukuze pepo yule kutoka kwa binti yake.
27 Yesu akamwambia, “Kwanza waache watoto watosheke, kwani sio haki kuwanyanganya watoto mkate wao na kuwapa mbwa.”
28 Lakini yeye akajibu, “Bwana hata mbwa walio chini ya meza wanakula mabaki ya chakula cha watoto.”
29 Kisha Yesu akamwambia, “kwa majibu haya unaweza kwenda nyumbani kwa amani: pepo mbaya amekwisha mtoka binti yako.”
30 Kwa hiyo akaenda nyumbani na akamkuta amelala akipumzika kitandani, na yule pepo tayari amekwisha mtoka.
Yesu Amponya Asiyesikia
31 Yesu akarudi kutoka katika eneo kuzunguka jiji la Tiro na akapita katika jiji la Sidoni hadi Ziwa Galilaya akipita katika jimbo la Dekapoli. 32 Pale watu wengine wakamletea mtu asiyeweza kusikia na tena aliyesema kwa shida. Nao wakamwomba Yesu amwekee mikono yake na kumponya.
33 Yesu akamchukua pembeni, kutoka katika kundi, na akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake. Kisha Yesu akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 Akaangalia juu mbinguni, akapumua na kumwambia “Efatha” yaani, “Funguka!” 35 Mara masikio ya mtu yule yakafunguka, na ulimi wake ukawa huru, na akaanza kuzungumza, vizuri.
36 Lakini kadiri jinsi alivyowaamuru wasimwambie mtu ndivyo walivyozidi kueneza habari hiyo. 37 Na watu wakashangazwa kabisa na kusema, “Yesu amefanya kila kitu vyema. Kwani amewafanya wale wasiosikia kusikia na wasiosema kusema.”
© 2017 Bible League International