Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
57 Wakati ulipotimia kwa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. 58 Majirani na jamaa zake waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa mwema kwake, walifurahi pamoja naye.
59 Mtoto alipofikisha umri wa siku nane, walikuja kumtahiri.[a] Walipotaka kumwita mtoto Zakaria kutokana na jina la baba yake. 60 Mama yake akasema, “Hapana, mtoto ataitwa Yohana.”
61 Lakini wao wakamwambia, “Hakuna jamaa yako hata mmoja mwenye jina hilo.” 62 Ndipo wakamfanyia ishara baba yake wakimwuliza jina alilotaka kumpa mtoto.
63 Zakaria akataka ubao wa kuandikia,[b] Kisha akaandika, “Jina lake ni Yohana.” Wote wakashangaa. 64 Mara hiyo hiyo mdomo wake ulifunguliwa na ulimi wake ukaachia, akaanza kuzungumza na kumsifu Mungu. 65 Majirani zao wakajawa hofu na watu katika sehemu zote za vilima katika jimbo la Yuda wakawa wanazungumza kuhusu jambo hili. 66 Watu wote waliosikia kuhusu mambo haya walijiuliza, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa kuwa nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
Zakaria Amsifu Mungu
67 Kisha Zakaria, baba yake Yohana, akajaa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema:
68 “Asifiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amekuja kuwasaidia
watu wake na kuwaweka huru.
69 Na ametuletea sisi Mwokozi Mwenye Nguvu,
kutoka katika ukoo wa mtumishi wake Daudi.
70 Hivi ndivyo alivyoahidi
kupitia manabii wake watakatifu tangu zamani.
71 Aliahidi kwa Agano kuwa atatuokoa na adui zetu
na milki za wote wanaotuchukia.
72 Ili kuonesha rehema kwa baba zetu,
na kulikumbuka agano lake takatifu aliloagana nao.
73 Agano hili ni kiapo alichomwapia
baba yetu Ibrahimu.
74 Alipoahidi kutuokoa kutoka katika nguvu za adui zetu,
ili tuweze kumwabudu Yeye bila hofu.
75 Katika namna iliyo takatifu na yenye haki
mbele zake siku zote za maisha yetu.
76 Sasa wewe, mtoto mdogo,
utaitwa nabii wa Mungu Aliye Juu Sana,
kwa sababu utamtangulia Bwana
kuandaa njia yake.
77 Utawaambia watu wake kwamba wataokolewa
kwa kusamehewa dhambi zao.
78 Kwa rehema ya upendo wa Mungu wetu,
siku mpya[c] itachomoza juu yetu kutoka mbinguni.
79 Kuwaangazia wale wanaoishi katika giza,
kwa hofu ya mauti,
na kuongoza hatua zetu
katika njia ya amani.”
80 Na hivyo mtoto Yohana akakua na kuwa na nguvu katika roho. Kisha akaishi maeneo yasiyo na watu mpaka wakati alipotokea hadharani akihubiri ujumbe wa Mungu kwa watu wa Israeli.
© 2017 Bible League International