Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo Aenda Yerusalemu
21 Baada ya kuwaaga wazee tulitweka tanga moja kwa moja kwenda kwenye kisiwa cha Kosi. Siku iliyofuata tulikwenda kisiwa cha Rhode na kutoka pale tulikwenda Patara. 2 Tulipata meli hapo iliyokuwa inakwenda maeneo ya Foeniki. Tukapanda meli na tukatweka tanga kuondoka.
3 Tulitweka tanga na kusafiri karibu na kisiwa cha Kipro. Tuliweza kukiona upande wa kaskazini, lakini hatukusimama. Tulisafiri mpaka katika jimbo la Shamu. Tulisimama Tiro kwa sababu meli ilitakiwa kupakua mizigo yake pale. 4 Tuliwapata wafuasi wa Bwana pale na tukakaa pamoja nao kwa siku saba. Walimuonya Paulo asiende Yerusalemu kwa sababu ya kile walichoambiwa na Roho Mtakatifu. 5 Lakini muda wetu wa kukaa pale ulipokwisha, tulirudi kwenye meli na kuendelea na safari yetu. Wafuasi wote, hata wanawake na watoto walikuja pamoja nasi pwani. Tulipiga magoti ufukweni sote, tukaomba, 6 na tukaagana. Kisha tukaingia melini, na wafuasi wa Bwana wakarudi nyumbani.
7 Tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro na kwenda katika mji wa Ptolemai. Tuliwasalimu waamini pale na kukaa nao kwa siku moja. 8 Siku iliyofuata tuliondoka Ptolemai na kwenda katika mji wa Kaisaria. Tulikwenda nyumbani kwa Filipo na kukaa kwake, alikuwa mhubiri wa Habari Njema. Alikuwa mmoja wa wasaidizi saba.[a] 9 Alikuwa na mabinti wanne mabikira waliokuwa na karama ya kutabiri.
10 Baada ya kuwa pale kwa siku kadhaa, nabii aliyeitwa Agabo alikuja kutoka Uyahudi. 11 Alikuja Kwetu na kuazima mkanda wa Paulo. Aliutumia mkanda huo na akajifunga mikono na miguu yake mwenyewe. Kisha akasema, “Roho Mtakatifu ananiambia, ‘Hivi ndivyo ambavyo Wayahudi walioko Yerusalemu watamfunga mtu anayeuvaa mkanda[b] huu. Kisha watamkabidhi kwa watu wasiomjua Mungu.’”
12 Tuliposikia hili, sisi na wafuasi wengine pale tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu. 13 Lakini Paulo alisema, “Kwa nini mnalia na kunihuzunisha? Niko radhi kufungwa Yerusalemu. Niko tayari hata kufa kwa ajili ya jina la Bwana Yesu!”
14 Hatukuweza kumshawishi asiende Yerusalemu. Hivyo tuliacha kumsihi na tukasema, “Tunaomba lile alitakalo Bwana lifanyike.”
15 Baada ya hili, tulijiandaa na kuelekea Yerusalemu. 16 Baadhi ya Wafuasi wa Yesu kutoka Kaisaria walikwenda pamoja nasi. Wafuasi hawa walitupeleka nyumbani kwa Mnasoni, mtu kutoka Kipro, ambaye alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kuwa wafuasi wa Yesu. Walitupeleka nyumbani kwake ili tukae pamoja naye.
© 2017 Bible League International