Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Kushindwa kwa Shetani
7 Miaka elfu moja itakapokwisha, Shetani ataachiwa huru kutoka kwenye gereza lake. 8 Atatoka na kwenda kuwadanganya mataifa katika dunia yote, mataifa yajulikanayo kama Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya watu kwa ajili ya vita. Kutakuwa watu wengi wasiohesabika kama mchanga katika ufukwe wa bahari.
9 Nililiona jeshi la Shetani likitembea na kujikusanya ili kuizingira kambi ya watu wa Mungu na mji anaoupenda Mungu. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuliteketeza jeshi la Shetani. 10 Na Shetani, yule aliyewadanganya watu hawa, alitupwa kwenye ziwa la moto pamoja na mnyama na nabii wa uongo. Watateseka kwa maumivu usiku na mchana milele na milele.
Watu wa Dunia Wahukumiwa
11 Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe. Nikamwona aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha enzi. Dunia na anga vikamkimbia na kutoweka. 12 Na nikaona wale waliokufa, wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi na vitabu vilifunguliwa. Na kitabu cha uzima kilifunguliwa pia. Watu walihukumiwa kwa yale waliyotenda, kama yalivyoandikwa katika vitabu.
13 Bahari ikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Mauti na kuzimu zikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Watu wote hawa walihukumiwa kutokana na matendo yao. 14 Mauti na kuzimu vilitupwa kwenye ziwa la moto. Ziwa hili la moto ni mauti ya pili. 15 Na yeyote ambaye jina lake halikuonekana limeandikwa kwenye kitabu cha uzima alitupwa kwenye ziwa la moto.
© 2017 Bible League International