Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mwili wa Kristo
12 Mtu ana mwili mmoja, lakini una viungo vingi. Kuna viungo vingi, lakini viungo vyote hivyo ni mwili mmoja. Kristo yuko vivyo hivyo pia. 13 Baadhi yetu ni Wayahudi na baadhi yetu si Wayahudi; baadhi yetu ni watumwa na baadhi yetu ni watu tulio huru. Lakini sisi sote tulibatizwa ili tuwe sehemu ya mwili mmoja kwa njia ya Roho mmoja. Nasi tulipewa[a] Roho mmoja.
14 Na mwili wa mtu una viungo zaidi ya kimoja. Una viungo vingi. 15 Mguu unaweza kusema, “Mimi si mkono, na hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kusema hivi hakutafanya mguu usiwe kiungo cha mwili. 16 Sikio linaweza kusema, “Mimi si jicho, hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kwa kusema hivi hakutafanya sikio lisiwe kiungo cha mwili. 17 Ikiwa mwili wote ungekuwa jicho, usingeweza kusikia. Ikiwa mwili wote ungekuwa sikio, usingeweza kunusa kitu chochote. 18-19 Ikiwa viungo vyote vya mwili vingekuwa kiungo kimoja, mwili usingekuwepo. Kama jinsi ilivyo, Mungu aliweka viungo katika mwili kama alivyotaka. Alikipa kila kiungo sehemu yake. 20 Hivyo kuna viungo vingi, lakini kuna mwili mmoja tu.
21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sikuhitaji!” Na kichwa hakiwezi kuuambia mguu, “sikuhitaji!” 22 Hapana, viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu zaidi, ndivyo vilivyo na umuhimu zaidi. 23 Na viungo ambavyo tunadhani kuwa vina umuhimu mdogo ndivyo tunavitunza kwa heshima kubwa. Na tunavitunza kwa kuvifunika kwa uangalifu maalum viungo vya mwili tusivyotaka kuvionesha. 24 Viungo vinavyopendeza zaidi visipofunikwa havihitaji matunzo haya maalum. Lakini Mungu aliuunganisha mwili pamoja na akavipa heshima zaidi viungo vilivyohitaji hadhi hiyo. 25 Mungu alifanya hivi ili mwili wetu usigawanyike. Mungu alitaka viungo vyote tofauti vitunzane kwa usawa. 26 Ikiwa kiungo kimoja cha mwili kinaugua, basi viungo vyote vinaugua pamoja nacho. Au ikiwa kiungo kimoja kinaheshimiwa, basi viungo vingine vyote vinashiriki heshima ya kiungo hicho.
27 Ninyi nyote kwa pamoja ni mwili wa Kristo. Kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo.
© 2017 Bible League International