Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Filipo Amfundisha Mtu Kutoka Ethiopia
26 Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jiandae na uende kusini katika barabara ya jangwani inayoteremka kutoka Yerusalemu kwenda Gaza.”
27 Filipo alijiandaa na kwenda. Akiwa njiani alimwona mwanaume kutoka Ethiopia. Alikuwa towashi na ofisa muhimu wa Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa na mweka hazina mkuu wa malkia. Mtu huyu alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu. 28 Na alikuwa anarudi Ethiopia. Alikuwa ameketi katika gari lake la kukokotwa na farasi akiwa anasoma kitabu cha nabii Isaya.
29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye gari hilo na uwe karibu yake.” 30 Hivyo Filipo akaenda karibu na gari, akamsikia mtu yule akisoma kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Unaelewa unachosoma?”
31 Yule mtu akajibu, “Nitaelewaje? Ninahitaji mtu wa kunifafanulia.” Ndipo akamwomba Filipo apande garini na aketi pamoja naye. 32 Sehemu ya Maandiko aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:
“Alikuwa kama kondoo
anayepelekwa kwa mchinjaji.
Alikuwa kama mwana kondoo asivyopiga kelele
anapokatwa manyoya yake.
Hakusema kitu.
33 Alidhalilishwa,
na kunyimwa haki zake zote.
Maisha yake duniani yamekoma.
Hivyo hakutakuwa simulizi yoyote kuhusu wazaliwa wake.”(A)
34 Afisa[a] akamwambia Filipo, “Tafadhali niambie, nabii anazungumza kuhusu nani? Anazungumza kuhusu yeye mwenyewe au mtu mwingine?” 35 Filipo akaanza kuzungumza. Alianzia na Andiko hili na kumwambia mtu yule Habari Njema kuhusu Yesu.
36 Walipokuwa wanasafiri waliyakuta maji mahali fulani. Afisa akasema, “Tazama! Hapa kuna maji! Nini kinanizuia nisibatizwe?” 37 [b] 38 Ndipo Afisa akaamuru gari lake lisimame. Wote wawili, Filipo na Afisa, wakatelemka wakaingia kwenye maji na Filipo akambatiza towashi. 39 Walipotoka kwenye maji, Roho wa Bwana akamchukua Filipo; afisa hakumwona Filipo tena. Afisa aliendelea na safari yake kurudi nyumbani, akiwa mwenye furaha sana. 40 Lakini Filipo alionekana katika mji ulioitwa Azoto. Alikuwa akienda kwenye mji wa Kaisaria. Aliwahubiri watu Habari Njema katika miji yote wakati anasafiri kutoka Azoto kwenda Kaisaria.
Upendo Hutoka kwa Mungu
7 Wapenzi rafiki, tunatakiwa tupendane sisi kwa sisi, kwa sababu upendo watoka kwa Mungu. Yeyote apendae amefanyika mwana wa Mungu. Na kila apendae anamfahamu Mungu. 8 Kila asiyependa hamfahamu Mungu, kwa sababu Mungu ni Pendo. 9 Hivi ndivyo Mungu alivyo tuonyesha pendo lake sisi: Alimtuma mwanawe wa pekee ulimwenguni kutupatia sisi uzima katika yeye. 10 Upendo wa kweli ni upendo wa Mungu kwa ajili yetu, si upendo wetu kwa Mungu. Alimtuma mwanawe kama njia ya kuziondoa dhambi zetu.
11 Hivyo ndivyo Mungu atupendavyo, rafiki wapenzi! Kwa hiyo tupendane sisi kwa sisi. 12 Hakuna aliyemwona Mungu. Ila tukipendana sisi kwa sisi, Mungu anaishi ndani yetu. Kama tukipendana sisi kwa sisi, Upendo wa Mungu unafikia shabaha yake na unafanywa kamili ndani yetu.
13 Twatambua kuwa tunaishi katika Mungu na mungu ndani yetu. Twalitambua hilo kwa sababu ametupa Roho wake. 14 Tumeona kuwa Baba alimtuma mwanaye aje kuwa Mwokozi wa ulimwengu, na hili ndilo tunalowaambia watu sasa. 15 Yeyote anayesema, “Naamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu,” huyo ni mtu anayeishi ndani ya Mungu, na Mungu anaishi ndani ya mtu huyo. 16 Hivyo twalifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu, na tunalitumainia pendo hilo.
Mungu ni pendo. Kila anae ishi katika pendo anaishi ndani ya Mungu, na Mungu ndani yao. 17 Kama pendo la Mungu limekamilishwa ndani yetu, tunaweza kuwa bila hofu siku ambayo Mungu atahukumu ulimwengu. Hatutakuwa na hofu, kwa sababu katika ulimwengu huu tunaishi kama Yesu.[a] 18 Palipo na upendo wa Mungu, hakuna hofu, kwa sababu upendo wa Mungu ulio kamili unaondoa hofu. Ni hukumu yake ndiyo inayomfanya mtu kuwa na hofu. Hivyo pendo lake halikamilishwi kwa mtu ambaye ndani yake kuna hofu.
19 Tunapenda kwa sababu Mungu alitupenda sisi kwanza. 20 Kama tukisema kuwa tunampenda Mungu na tunamchukia mmojawapo wa kaka na dada zetu katika familia ya Mungu, basi sisi tu waongo. Kama hatuwezi kumpenda mtu tunayemwona, tutawezaje kumpenda Mungu, ambaye hata hatujamwona. 21 Mungu ametupa amri hii: Kama tunampenda Mungu, Ni lazima pia tupendane sisi kwa sisi kama kina kaka na kina dada.
Yesu ni Kama Mzabibu
15 Yesu akasema, “Mimi ndiye mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Yeye hulikata kutoka kwangu kila tawi lisilozaa matunda.[a] Pia hupunguza majani katika kila tawi linalozaa matunda ili kuliandaa liweze kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmewekwa tayari[b] kwa ajili ya kuzaa matunda[c] kutokana na mafundisho yale niliyowapa. 4 Hivyo mkae mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nitakaa nikiwa nimeunganishwa kwenu. Hakuna tawi linaloweza kuzaa matunda likiwa liko peke yake. Ni lazima liwe limeunganishwa katika mzabibu. Ndivyo ilivyo hata kwenu. Hamwezi kutoa matunda mkiwa peke yenu. Ni lazima muwe mmeunganishwa kwangu.
5 Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Mtatoa matunda mengi sana mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nimeunganishwa kwenu. Lakini mkitenganishwa mbali nami hamtaweza kufanya jambo lo lote. 6 Kama hamtaunganishwa nami, basi mtakuwa sawa na tawi lililotupwa pembeni nanyi mtakauka. Matawi yote yaliyokufa jinsi hiyo hukusanywa, hutupwa katika moto na kuchomwa. 7 Hivyo ninyi mbaki mmeunganishwa nami, na mfuate mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, mnaweza kuomba kitu chochote mnachohitaji, nanyi mtapewa. 8 Ninyi mdhihirishe kuwa mmekuwa wafuasi wangu kwa kutoa matunda mengi. Kwani hiyo itamletea Baba utukufu.[d]
© 2017 Bible League International