Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Shukrani kwa Rehema za Mungu
12 Ninamshukuru Kristo Yesu Bwana wetu kwa sababu aliniamini na kunipa kazi hii ya kumtumikia. Yeye hunitia nguvu ya kufanya kazi hii. 13 Hapo zamani nilimtukana Kristo. Nikiwa mtu mwenye majivuno na mkorofi, niliwatesa watu wake. Lakini Mungu alinihurumia kwa sababu sikujua nilichokuwa nafanya. Nilifanya hayo kabla sijaamini. 14 Lakini Bwana wetu alinipa kiwango kikubwa cha neema yake. Na pamoja na neema hiyo imani na upendo ulio katika Kristo Yesu vilifuata.
15 Huu ndiyo usemi wa kweli unaopaswa kukubaliwa pasipo kuuliza maswali; kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, nami ni mbaya zaidi ya wote. 16 Lakini nilipata rehema kwa sababu ili Kristo Yesu aweze kunitumia, mimi mtenda dhambi kuliko wote, ili kuonesha uvumilivu wake usio na kikomo. Alitaka niwe mfano kwa wale ambao wangemwamini na kupata uzima wa milele. 17 Heshima na utukufu kwa mfalme anayetawala milele. Hawezi kuharibiwa wala kuonekana. Heshima na utukufu apewe Mungu wa pekee milele na milele, Amina.
18 Timotheo wewe ni mwanangu mwenyewe kwa sababu ya ushirika wetu wa imani ya kweli. Ninayokuambia kuyatenda yanakubaliana na unabii[a] ambao ulisemwa juu yako hapo zamani. Nataka uukumbuke unabii huo na kupigana vita vizuri vya imani. 19 Endelea kumwamini Mungu na kutenda yale unayojua kuwa ni sahihi. Watu wengine hawajatenda haya, na imani yao sasa imeharibiwa. 20 Himenayo na Iskanda ni mfano wa watu hao. Nimewakabidhi kwa Shetani ili wafundishwe kutosema kinyume cha Mungu.
© 2017 Bible League International