Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo na Barnaba Wakiwa Ikonia
14 Paulo na Barnaba walikwenda katika mji wa Ikonia. Kama walivyofanya Antiokia, waliingia katika sinagogi la Kiyahudi. Walizungumza na watu pale. Walizungumza kwa ushawishi sana kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wengi waliamini walichosema. 2 Lakini Baadhi ya Wayahudi hawakuamini. Wayahudi hao walisema mambo yaliyowafanya wasio Wayahudi kukasirika na kuwa kinyume na waamini.
3 Hivyo Paulo na Barnaba walikaa Ikonia kwa muda mrefu, na walihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. Waliwahubiri watu kuhusu neema ya Mungu. Bwana alithibitisha kwamba kile walichosema ni kweli kwa ishara na maajabu yaliyofanyika kufanyika kupitia wao. 4 Lakini baadhi ya watu katika mji wakakubaliana na Wayahudi ambao hawakuwaamini Paulo na Barnaba. Baadhi walikubaliana na mafundisho ya mitume. Hivyo mji uligawanyika.
5 Baadhi ya Wayahudi, viongozi wao na baadhi ya watu wasio wayahudi, walidhamiria kuwaumiza Paulo na Barnaba. Walitaka kuwaua kwa kuwapiga kwa mawe. 6 Paulo na Barnaba walipotambua kuhusu hili, wakaondoka katika mji huo. Walikwenda Listra na Derbe, miji katika Likonia na maeneo yanayozunguka Likonia. 7 Wakahubiri Habari Njema huko pia.
© 2017 Bible League International