Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo Amtembelea Yakobo
17 Ndugu na dada wa Yerusalemu walitukabisha kwa furaha sana walipotuona. 18 Siku iliyofuata Paulo alikwenda pamoja nasi kumtembelea Yakobo. Wazee wote walikuwepo pia. 19 Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwaambia hatua kwa hatua yote ambayo Mungu aliyatenda katikati ya watu wasio Wayahudi kupitia huduma yake.
20 Viongozi waliposikia hili, wakamsifu Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu yetu, unaweza kuona maelfu ya Wayahudi wamekuwa waamini, lakini wanadhani ni muhimu kutii Sheria ya Musa. 21 Wameambiwa kuwa unawafundisha Wayahudi wanaoishi katika majimbo yasiyo ya Kiyahudi kuacha kufuata Sheria ya Musa. Wamesikia kuwa unawaambia wasiwatahiri watoto wao na wasifuate desturi zetu.
22 Tufanye nini? Wafuasi wayahudi hapa watajua kuwa umekuja. 23 Hivyo tutakwambia nini cha kufanya: Watu wanne miongoni mwa watu wetu wameweka nadhiri[a] kwa Mungu. 24 Wachukue watu hawa walio pamoja nawe na ushiriki katika ibada ya utakaso.[b] Lipia gharama zao ili wanyoe nywele za vichwa vyao. Hili litathibitisha kwa kila mmoja kuwa mambo waliyosikia kuhusu wewe si sahihi. Watajua kuwa wewe mwenyewe unaitii Sheria ya Musa katika maisha yako.
25 Tumekwisha watumia barua waamini wasio Wayahudi kuwaambia ambayo hawapaswi kufanya:
‘Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu.
Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama zilizo na damu ndani yake.
Wasijihusishe na uzinzi.’”
Paulo Akamatwa
26 Hivyo Paulo akawachukua wale watu wanne aliokuwa pamoja nao. Siku iliyofuata alishiriki kwenye ibada ya kuwatakasa. Kisha akaenda eneo la Hekalu na kutangaza siku ya mwisho ambapo kipindi cha utakaso kitakwisha na kwamba sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wa watu hao siku hiyo.
© 2017 Bible League International