Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Kuhusu Vyakula Vinavyotolewa kwa Sanamu
8 Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu nyama iliyotolewa sadaka[a] kwa sanamu. Ni kweli kuwa “Sote tuna ujuzi”, kama mnavyosema. Lakini ujuzi huu unawajaza watu majivuno. Upendo ndiyo unaolisaidia kanisa kuwa imara. 2 Wale wanaodhani kuwa wanajua jambo fulani bado hawajui chochote kwa namna inavyopaswa. 3 Lakini Mungu anamjua mtu anayempenda.
4 Hivyo sasa vipi kuhusu kula nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu? Tunajua kuwa “sanamu si lolote katika ulimwengu” huu na tunajua kuwa “kuna Mungu mmoja tu”. 5 Baadhi ya watu husema kuwa kuna miungu wanaoishi mbinguni na miungu wengine huishi duniani. Hata kama kuna “miungu” na “mabwana” wanaoaminiwa na watu, hilo si muhimu kwetu. 6 Tuna Mungu mmoja tu, na ambaye ndiye Baba yetu. Vitu vyote vilitoka kwake nasi tunaishi kwa ajili yake. Na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo. Vitu vyote viliumbwa kupitia yeye, nasi tunaishi kwa ajili yake.
7 Lakini si watu wote wanaojua hili. Baadhi ya watu walikuwa na tabia ya kuabudu sanamu huko nyuma. Hivyo wanapokula nyama, bado wanahisi kuhukumiwa kana kwamba wanakula nyama iliyotolewa kwa sanamu. Hawana uhakika ikiwa ni sahihi kula nyama. 8 Lakini chakula hakitatuweka karibu na Mungu. Kukataa kula hakutufanyi tumpendeze kidogo Mungu wala kula hakutuweki karibu na Mungu.
9 Lakini iweni makini na uhuru wenu. Uhuru wa kula kitu unaweza kuwafanya walio na mashaka wakaanguka katika dhambi kwa kula vyakula hivyo. 10 Mnaelewa kuwa inaruhusiwa kula kitu chochote, hivyo unaweza kula hata katika hekalu la sanamu. Lakini hilo linaweza kumfanya mtu mwenye mashaka akaona kuwa kula chakula kama hicho ni kitendo cha kuabudu sanamu. 11 Hivyo ndugu huyu aliye dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, anaweza akaangamizwa kwa sababu ya uelewa wako ulio mzuri zaidi. 12 Unapomtenda dhambi kinyume cha ndugu zako walio katika Kristo kwa namna hii na unawaumiza kwa kuwafanya wafanye mambo wanayoyachukulia kuwa mabaya, nawe pia unamtenda dhambi Kristo. 13 Hivyo ikiwa chakula ninachokula kinamfanya mwamini mwingine kutenda dhambi, siwezi kula chakula hicho tena. Nitaacha kula chakula hicho ili nisimfanye ndugu yangu atende dhambi.
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Mchafu
(Lk 4:31-37)
21 Kisha Yesu na wafuasi wake waliingia Kapernaumu. Siku ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na akaanza kuwafundisha watu. 22 Walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.[a] 23 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Naye mara alipiga kelele na kusema, 24 “Unataka nini kwetu, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.”
25 Lakini Yesu akamkemea na kumwambia, “Nyamaza kimya, na kisha umtoke ndani yake.” 26 Ndipo roho yule mchafu akamfanya mtu yule atetemeke. Kisha akatoa sauti kubwa na kisha akamtoka.
27 Kila mmoja akashangazwa sana kiasi cha kuwafanya waulizane, “Hii ni nini? Ni mafundisho ya aina mpya, na mtu yule anafundisha kwa mamlaka! Yeye huwapa amri pepo wachafu nao wanamtii!” 28 Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea haraka katika eneo lote la Galilaya.
© 2017 Bible League International