Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Yesu Atarudi
3 Rafiki zangu, hii ni barua yangu ya pili kuwaandikia. Barua zote mbili nimewaandikia ili kusaidia fikra zenu njema zikumbuke kitu. 2 Ninataka mkumbuke maneno ambayo manabii watakatifu walisema huko nyuma. Na mkumbuke amri ambayo Bwana na Mwokozi wetu aliwapa. Aliwapa amri hiyo kupitia mitume wake waliowafundisha.
3 Ni muhimu kwenu kuelewa kitakachotokea siku za mwisho. Watu watawacheka kwa yale mliyofundishwa. Wataishi kwa kufuata maovu wanayotaka kufanya. 4 Watasema, “Yesu aliahidi kuwa atarudi. Yuko wapi? Baba zetu wamekufa, lakini ulimwengu unaendelea kama ambavyo umekuwa tangu ulipoumbwa.”
5 Lakini watu hawa hawataki kukumbuka kilichotokea zamani. Anga ilikuwepo, na Mungu aliiumba dunia kwa kutumia maji. Hili lilitokea kwa neno la Mungu. 6 Kisha ulimwengu uliangamizwa kwa maji wakati wa gharika. 7 Na neno hilo hilo la Mungu linaiweka anga na dunia tuliyonayo sasa. Vimewekwa ili vichomwe moto. Vimewekwa kwa ajili ya siku ya hukumu na kuangamia kwa watu wote walio kinyume na Mungu.
© 2017 Bible League International