Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
11 Na wafanya biashara wa dunia watalia na kuhuzunika kwa ajili yake. Watahuzunika kwa sababu hakutakuwa hata mmoja wa kununua vitu wanavyouza; 12 dhahabu, fedha, vito, lulu, nguo za kitani safi, nguo za zambarau, hariri na nguo nyekundu, aina zote za mti wa udi, na aina zote za vitu vilivyotengenezwa kutokana na pembe za wanyama, miti ya thamani, shaba, chuma, na marimari. 13 Na mdalasini, viungo, uvumba, marhamu, ubani, mvinyo, mafuta ya mzeituni, unga safi, ngano, ng'ombe, kondoo, farasi, magari na watumwa, ndiyo hata maisha ya watu. Wafanya biashara watalia na kusema:
14 “Ee Babeli, mambo mazuri uliyoyataka yamekuacha.
Utajiri wako wote na vitu vya fahari vimetoweka.
Hautakuwa navyo tena.”
15 Wafanya biashara wataogopa mateso yake na watakaa mbali naye. Hawa ni wale waliotajirika kwa kumwuzia vitu hivyo. Watalia na kuhuzunika. 16 Watasema:
“Inatisha! Inatisha kwa mji mkuu!
Alivalishwa kitani safi;
alivaa zambarau na nguo nyekundu.
Alikuwa anang'aa kwa sababu ya dhahabu, vito na lulu!
17 Utajiri wote huu umeteketezwa kwa saa moja!”
Kila nahodha, wote ambao husafiri katika meli, mabaharia na wote ambao hupata pesa kutokana na bahari walisimama mbali na Babeli. 18 Waliuona moshi wa kuungua kwake. Walilia kwa sauti, “Hakukuwa na mji kama mji huu mkuu!” 19 Walirusha mavumbi juu ya vichwa vyao na kulia kwa sauti kuu kuonesha huzuni kuu waliyokuwa nayo. Walisema:
“Inatisha! Inatisha sana kwa mji mkuu!
Wote waliokuwa na meli baharini walitajirika kwa sababu ya utajiri wake!
Lakini umeteketezwa katika saa moja!
20 Ufurahi kwa sababu ya hili, Ee mbingu!
Furahini, watakatifu wa Mungu, mitume na manabii!
Mungu amemhukumu kwa sababu ya kile alichowatendea ninyi.”
© 2017 Bible League International