Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Miili Yenu Itumike kwa Ajili ya Utukufu wa Mungu
12 Mtu mmoja anaweza kusema, “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote.” Nami ninawaambia ya kuwa si vitu vyote vilivyo na manufaa. Hata kama ni kweli kuwa “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote,” Sitaruhusu kitu chochote kinitawale kama vile ni mtumwa. 13 Mmoja wenu anasema, “Chakula ni kwa ajili ya tumbo na tumbo ni kwa ajili ya chakula, na Mungu ataviteketeza vyote.” Hiyo ni dhahiri, lakini mwili si kwa ajili ya zinaa, bali kwa ajili ya Bwana, na Bwana ni kwa ajili ya mwili. 14 Na Mungu ataifufua pia miili yetu kutoka kwa wafu kwa nguvu yake, kama alivyomfufua Bwana Yesu. 15 Hakika mnajua kuwa miili yenu ni sehemu ya Kristo mwenyewe. Hivyo sitakiwi kamwe kuchukua sehemu ya Kristo na kuiunganisha na kahaba! 16 Maandiko yanasema, “Watu wawili watakuwa mmoja.”(A) Hivyo mnapaswa kujua kuwa kila aliyeungana na kahaba, amekuwa mwili mmoja na kahaba. 17 Lakini aliyeungana na Bwana, yu mmoja naye katika roho.
18 Hivyo ikimbieni dhambi ya uzinzi. Mnasema kuwa, “Kila dhambi ni kitu kilichomo katika akili tu haihusiki na mwili.” Lakini ninawaambia, anayetenda dhambi ya uzinzi anautendea dhambi mwili wake mwenyewe. 19 Nina uhakika mnajua kuwa mwili wenu ni hekalu[a] kwa ajili ya Roho Mtakatifu mliyepewa na Mungu na Roho Mtakatifu anaishi ndani yenu. Hamjimiliki ninyi wenyewe. 20 Mungu alilipa gharama kubwa ili awamiliki. Hivyo mtukuzeni Yeye kwa kutumia miili yenu.
43 Kesho yake Yesu akaamua kwenda Galilaya. Huko alikutana na Filipo na kumwambia, “Nifuate.” 44 Filipo alikuwa mwenyeji wa mji wa Bethsaida, kama alivyokuwa Andrea na Petro. 45 Filipo akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona mtu ambaye habari zake ziliandikwa na Musa katika sheria. Pia Manabii waliandika habari juu ya mtu huyu. Yeye ni Yesu, mwana wa Yusufu. Naye anatoka mjini Nazareti!”
46 Lakini Nathanaeli akamwambia Filipo, “Nazareti! Je, inawezakana kupata kitu chochote chema kutoka Nazareti?”
Filipo akajibu, “Njoo uone.”
47 Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake na papo hapo akasema, “Mtu huyu anayekuja ni Mwisraeli halisi, ambaye unayeweza kumwamini.”[a]
48 Nathanaeli akamwuliza Yesu, “Umenifahamu kwa namna gani?”
Yesu akamjibu, “Nilikuona pale ulipokuwa chini ya mtini,[b] kabla Filipo hajakueleza habari zangu.”
49 Kisha Nathanaeli akasema, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Nawe ni mfalme wa Israeli.” 50 Yesu akamwambia, “Je, umeyaamini haya kwa sababu nimekwambia kuwa nilikuona chini ya mtini? Utaona mambo makubwa zaidi ya haya.” 51 Kisha akasema, “Mniamini ninapowaambia kwamba mtaziona mbingu zimefunguka. Na mtawaona, ‘Malaika wa Mungu wakipanda juu na kushuka chini’[c] kwa ajili Mwana wa Adamu.”
© 2017 Bible League International