Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Wanawali Kumi
25 Nyakati hizo, ufalme wa Mungu utafanana na wanawali kumi waliokwenda kusubiri kuwasili kwa bwana arusi wakiwa na taa zao. 2 Watano kati yao walikuwa na hekima, na watano walikuwa wajinga. 3 Wanawali wajinga walichukua taa zao bila ya kubeba mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao. 4 Wanawali wenye hekima walichukua taa zao pamoja na mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao katika chupa. 5 Bwana arusi alipochelewa sana, walichoka na wote wakasinzia.
6 Usiku wa manane ulipofika, ikatangazwa, ‘Bwana arusi anakuja! Njooni mumlaki!’
7 Wasichana wote waliamka. Wakatayarisha taa zao. 8 Lakini wanawali wajinga wakawaambia wanawali wenye hekima, ‘Tupeni mafuta kiasi kwa sababu mafuta katika taa zetu yamekwisha.’
9 Wanawali wenye hekima wakajibu, ‘Hapana! Mafuta tuliyonayo hayatatutosha sisi sote. Lakini nendeni kwa wauza mafuta mkanunue.’
10 Hivyo wanawali wajinga wakaenda kununua mafuta. Walipoondoka, bwana arusi akafika. Wanawali waliokuwa tayari wakaingia kwenye sherehe ya arusi pamoja na bwana arusi. Kisha mlango ukafungwa.
11 Baadaye wanawali waliokwenda kununua mafuta wakarudi. Wakasema, ‘bwana, bwana! Fungua mlango tuingie.’
12 Lakini bwana arusi akajibu, ‘Kwa hakika hapana! Wala siwajui ninyi.’
13 Hivyo iweni tayari kila wakati. Hamjui siku wala muda ambao Mwana wa Adamu atakuja.
© 2017 Bible League International