Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
2 Wayahudi walipomsikia Paulo anazungumza kwa Kiaramu wakanyamaza. Kisha Paulo akasema,
3 “Mimi ni Myahudi, nilizaliwa katika mji wa Tarso katika jimbo la Kilikia. Nilikulia hapa katika mji huu. Nilikuwa mwanafunzi wa Gamalieli[a] ambaye kwa umakini alinifundisha kila kitu kuhusu sheria ya baba zetu. Daima nimekuwa na shauku ya kumheshimu Mungu, sawa na ninyi nyote hapa leo. 4 Niliwatesa watu walioifuata Njia. Baadhi yao hapa waliuawa kwa sababu yangu. Niliwakamata wanaume na wanawake na kuwaweka gerezani.
5 Kuhani mkuu na baraza lote la wazee wa Wayahudi wanaweza kuwathibitishia hili. Wakati mmoja viongozi hawa walinipa barua. Barua hizo waliandikiwa ndugu zetu Wayahudi katika mji wa Dameski. Nilikuwa naenda huko kuwakamata wafuasi wa Yesu na kuwaleta Yerusalemu ili waadhibiwe.
Paulo Aeleza Kuhusu Kuokolewa Kwake
6 Lakini kitu fulani kilinitokea nikiwa njiani kwenda Dameski. Ilipokuwa inakaribia mchana na nilikuwa karibu na mji wa Dameski. Ghafla mwanga kutoka mbinguni ulining'aria kunizunguka. 7 Nilianguka chini na nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli kwa nini unanitesa?’
8 Niliuliza, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ Sauti ikasema, ‘Mimi ni Yesu kutoka Nazareti, unayemtesa.’ 9 Watu waliokuwa pamoja nami hawakuisikia sauti lakini waliona mwanga.
10 Nilisema, ‘Nifanye nini Bwana?’ Bwana alinijibu, ‘Simama na uingie Dameski. Humo utawaambia yote niliyopanga uyafanye.’ 11 Sikuweza kuona kwa sababu mwanga ule angavu ulinilemaza macho. Hivyo wale watu waliokuwa pamoja nami waliniongoza kuingia mjini Dameski.
12 Alikuwepo mtu mmoja katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania.[b] Mtu huyu alikuwa mcha Mungu na aliitii Sheria ya Musa na Wayahudi wote walioishi kule walimheshimu. 13 Alikuja kwangu na kuniambia, ‘Sauli, ndugu yangu, tazama juu na uone tena!’ Ghafla niliweza kumwona.
14 Anania aliniambia, ‘Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu alikuchagua wewe tangu zamani kuujua mpango wake. Amekuchagua wewe kumwona Mwenye Haki wake na kusikia maneno kutoka kwake. 15 Utakuwa shahidi wake kwa watu wote. Utawaambia ulichoona na kusikia. 16 Sasa usisubiri zaidi. Simama, ubatizwe na usafishwe dhambi zako, mwamini Yesu ili akuokoe.’[c]
© 2017 Bible League International