Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Yesu Apelekwa Uhamishoni Misri
13 Baada ya wenye hekima kuondoka, malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto na kumwambia, “Damka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake ukimbilie Misri kwa sababu Herode amedhamiria kumwua mtoto na sasa atatuma watu kumtafuta. Na mkae Misri mpaka nitakapowaambia mrudi.”
14 Hivyo Yusufu alidamka na kutoka kwenda Misri akiwa na mtoto na mama yake. Nao waliondoka usiku. 15 Yusufu na familia yake walikaa huko Misri mpaka Herode alipofariki. Hili lilitukia ili maneno yaliyosemwa na nabii yatimie: “Nilimwita mwanangu atoke Misri.”(A)
Herode Aua Watoto wa Kiume Katika Mji wa Bethlehemu
16 Herode alipoona kuwa wenye hekima wamemfanya aonekane mjinga, alikasirika sana. Hivyo akatoa amri ya kuua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili au chini ya miaka hiyo katika mji wa Bethlehemu na vitongoji vyake. Herode alifahamu kutoka kwa wenye hekima kwamba walikuwa wameiona nyota miaka miwili kabla. 17 Hili likatimiza yale yaliyosemwa na Mungu kupitia nabii Yeremia aliposema:
18 “Sauti imesikika Rama,
sauti ya kilio na huzuni kuu.
Raheli akiwalilia watoto wake,
na amekataa kufarijiwa
kwa sababu watoto wake hawapo tena.”(B)
© 2017 Bible League International