Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Baadhi ya Wayahudi Wampinga Stefano
8 Mungu alimpa Stefano nguvu ya kutenda maajabu makuu na miujiza katikati ya watu. 9 Lakini baadhi ya Wayahudi pale waliotoka katika sinagogi la Watu Huru,[a] kama lilivyoitwa. Kundi hili lilijumuisha Wayahudi kutoka Kirene, Iskanderia, Kilikia na Asia. Walianza kubishana na Stefano. 10 Lakini Roho Mtakatifu alimwezesha kuzungumza kwa hekima. Maneno yake yalikuwa na nguvu hata Wayahudi hawa hawakuweza kubishana naye.
11 Hivyo wakawaambia baadhi ya watu waseme, “Tumemsikia Stefano akimtukana Musa na Mungu!” 12 Jambo hili liliwakasirisha sana watu, wazee wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Wakamkamata Stefano na kumpeleka mbele ya Baraza Kuu.
13 Wayahudi wakawaleta baadhi ya watu kwenye mkutano ili kusema uongo kuhusu Stefano. Watu hawa walisema, “Daima mtu huyu husema maneno kinyume na mahali hapa patakatifu na kinyume na Sheria ya Musa. 14 Tulimsikia akisema kwamba Yesu kutoka Nazareti atapaharibu mahali hapa na kubadilisha yale ambayo Musa aliyotuambia kufanya.” 15 Kila mtu aliyekuwa kwenye mkutano wa baraza alikuwa akimshangaa Stefano kwani uso wake ulionekana kama uso wa malaika.
51 Kisha Stefano akasema, “Enyi viongozi wa Kiyahudi mlio wakaidi! Mnakataa kumpa Mungu mioyo yenu na mnakataa hata kumsikiliza. Daima mko kinyume na Roho Mtakatifu. Baba zenu walikuwa vivyo hivyo, nanyi mko kama wao! 52 Walimtesa kila nabii aliyewahi kuishi. Waliwaua hata wale ambao zamani zilizopita walisema kwamba Mwenye Haki ilikuwa aje. Na sasa mmekuwa kinyume na Mwenye Haki na mmemwua. 53 Ninyi ndiyo mliipokea Sheria ya Mungu,[a] aliyoitoa kupitia malaika zake. Lakini hamtaki kuitii!”
Stefano Auawa
54 Waliokuwa kwenye mkutano wa baraza waliposikia maneno haya, walikasirika sana na wakamsagia meno Stefano kwa hasira. 55 Lakini Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama juu mbinguni, na kuuona utukufu wa Mungu. Alimwona Yesu amesimama upande wa kulia wa Mungu. 56 Stefano akasema, “Tazama! Naona mbingu zimefunguka. Na ninamwona Mwana wa Adamu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”
57 Kila mmoja pale akaanza kupiga kelele, wakaziba masikio yao kwa mikono yao. Wote kwa pamoja wakamvamia Stefano. 58 Wakamtoa nje ya mji na kuanza kumpiga kwa mawe. Mashahidi walioshuhudia uongo kinyume cha Stefano waliacha makoti yao kwa kijana aliyeitwa Sauli. 59 Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa.
© 2017 Bible League International