Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Malaika Watatu
6 Kisha nikaona malaika mwingine akipaa juu angani, akitangaza Habari Njema ya milele kwa watu waishio duniani, watu wa kila taifa, kabila, lugha na rangi. 7 Malaika akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na msifuni yeye. Wakati wa Mungu kuwahukumu watu wote umefika. Mwabuduni Mungu. Aliumba mbingu, dunia, bahari na chemichemi za maji.”
8 Kisha malaika wa pili akamfuata malaika wa kwanza na kusema, “Ameteketezwa! Mji mkuu Babeli umeteketezwa! Aliwafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.”
9 Malaika wa tatu aliwafuata malaika wawili wa kwanza. Malaika huyu wa tatu alisema kwa sauti kuu, “Mungu atawaadhibu wote wanaomwabudu mnyama na sanamu ya mnyama na kukubali kuwa na alama ya mnyama katika vipaji vya nyuso zao au kwenye mkono wao. 10 Watakunywa mvinyo wa ghadhabu ya Mungu.[a] Mvinyo huu umeandaliwa kwa nguvu zake zote katika kikombe cha ghadhabu ya Mungu. Watateseka kwa maumivu ya moto uwakao kwa kiberiti mbele ya malaika watakatifu na Mwanakondoo. 11 Na moshi kutokana na kuungua kwao utasimama milele na milele. Hakutakuwa mapumziko, usiku na mchana kwa wale wamwabuduo mnyama au sanamu yake au wale wavaao alama ya jina lake.” 12 Hii inamaanisha kuwa ni lazima watakatifu wa Mungu wawe na subira. Ni lazima wazitii amri za Mungu nakuendelea kumwamini Yesu.
13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Liandike hili: Kuanzia sasa heri wale wanaokufa wakiwa wa Bwana.”
Roho Mtakatifu anasema, “Ndiyo, hilo ni kweli. Watapumzika kutokana na kazi yao ngumu. Yale waliyotenda yatakaa pamoja nao.”
© 2017 Bible League International