Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
8 Malaika wa nne akaimimina bakuli yake juu ya jua. Jua lilipewa nguvu kuwachoma watu kwa moto. 9 Watu wakaungua kwa joto kali. Wakalilaani jina la Mungu, mwenye mamlaka juu ya mapigo haya. Lakini walikataa kubadili mioyo na maisha yao, na kumpa Mungu utukufu.
10 Malaika wa tano akaimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha mnyama. Giza likaufunika ufalme wa mnyama. Watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu. 11 Wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majipu waliyokuwa nayo. Lakini walikataa kubadili mioyo yao na kuyaacha maovu wanayotenda.
12 Malaika wa sita akaimimina bakuli yake juu ya mto mkuu Frati. Maji yaliyokuwa mtoni yakakauka. Hili likaandaa njia kwa ajili ya watawala kutoka mashariki kuweza kupita. 13 Kisha nikaona roho chafu tatu zilizoonekana kama vyura. Walitoka katika kinywa cha joka, kinywa cha mnyama, na kinywa cha nabii wa uongo. 14 Roho hizi chafu ni roho za mapepo. Zina nguvu za kutenda miujiza.[a] Nazo huenda kwa watawala wa ulimwengu wote na kuwakusanya kwa ajili ya mapigano siku ile Mungu Mkuu Mwenye Nguvu.
15 “Sikilizeni! Nitakuja kama mwizi wakati msioutarajia. Heri watakaokuwa macho na waliovaa nguo zao. Hawatakwenda wakiwa uchi na kuona aibu watakapoonwa na watu.”
16 Ndipo roho chafu zikawakusanya pamoja watawala pamoja mahali ambapo kwa Kiebrania panaitwa “Armagedoni”.
17 Malaika wa saba akaimimina bakuli yake angani. Sauti kuu ikatoka hekaluni katika kiti cha enzi. Ikasema, “Imekwisha!” 18 Kisha kukawa na mwako wa radi, kelele, ngurumo za radi na tetemeko kuu la nchi. Hili lilikuwa tetemeko kuu kuwahi kutokea tangu watu walipokuwepo duniani. 19 Mji mkuu ukagawanyika vipande vitatu. Miji ya mataifa ikaharibiwa. Na Mungu hakusahau kuuadhibu Babeli Mkuu. Aliupa mji ule kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu yake kuu. 20 Kila kisiwa kikatoweka na milima ikasawazika, hakukuwa milima yoyote tena. 21 Mvua yenye mawe makubwa kutoka mbinguni ikawanyeshea watu. Mawe haya yalikuwa na uzito wa kilo 40[b] kila jiwe. Watu wakamlaani Mungu kwa sababu ya mvua hii ya mawe. Hali hiyo Ilitisha sana.
© 2017 Bible League International