Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
6 Bali sasa Timotheo amerudi kutoka kwenu na kutueleza juu ya uaminifu wenu na upendo wenu. Ametueleza kuwa mmeendelea kuwa na kumbukumbu njema juu yetu kama mfano kwenu. Na amesema kuwa mnatamani sana kutuona tena. Hivyo ndivyo ilivyo kwetu pia tunatamani sana kuwaona ninyi. 7 Kwa hiyo, ndugu zangu, tunatiwa moyo sana kwa ajili ya uaminifu wenu. Tunapata mateso na masumbufu mengi, lakini bado tunatiwa moyo nanyi. 8 Kwa kuwa sasa tuna maisha mapya tunapata utimilifu ikiwa imani yenu katika Bwana inaendelea kuwa imara. 9 Tuna furaha tele mbele za Mungu wetu kwa ajili yenu! Lakini hatuwezi kumshukuru Mungu inavyopasa kwa furaha ile yote tuliyo nayo. 10 Usiku na mchana tuliendelea kuomba kwa mioyo yetu yote kwamba tuweze kuja huko na tuwaone tena. Tunataka kuwapa kila mnachohitaji ili imani yenu iwe timilifu.
11 Tunaomba kwamba Mungu wetu aliye Baba yetu, na Bwana Yesu wataiongoza njia yetu kuja kwenu. 12 Tunaomba kuwa Bwana ataufanya upendo wenu uendelee kukua. Tunaomba kuwa atawapa kupendana zaidi na zaidi miongoni mwenu na kwa watu wote. Tunaomba kuwa mtampenda kila mmoja kwa namna ile ile ambayo sisi tuliwapenda ninyi. 13 Hii itaongeza hamu yenu ya kutenda yaliyo haki, na mtakuwa watakatifu msio na kosa mbele za Mungu wetu na baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapo kuja na watakatifu[a] wake wote.
© 2017 Bible League International