Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mlio wa Tarumbeta ya Sita
13 Malaika wa sita alipopuliza tarumbeta yake, nilisikia sauti ikitoka katika pembe[a] zilizo katika pembe[b] nne za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu. 14 Ikamwambia malaika wa sita aliyekuwa na tarumbeta, “Wafungue huru malaika wanne waliofungwa pembezoni mwa mto mkuu Frati.” 15 Malaika hawa wanne walikuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hii, siku hii, mwezi na mwaka huu. Malaika waliachwa huru ili waue theluthi moja ya watu duniani. 16 Nikasikia kuwa idadi ya askari waliowaendesha farasi walikuwa milioni mia mbili.
17 Katika maono yangu, niliona farasi na waendesha farasi wakiwa juu ya farasi. Walionekana hivi: Walivaa dirii za chuma vifuani mwao zilizokuwa za rangi nyekundu, rangi ya bahari iliyoiva na za rangi ya njano kama baruti. Vichwa vya farasi vilionekana kama vichwa vya simba. Farasi walikuwa wanatoa moto, moshi na baruti katika vinywa vyao. 18 Theluthi ya watu wote duniani walikufa kutokana na mapigo haya matatu yaliyokuwa yanatoka vinywani mwa farasi: moto, moshi na baruti. 19 Nguvu ya farasi ilikuwa kwenye midomo na mikia yao. Mikia yao ilikuwa kama nyoka walio na vichwa vya kuwauma na kuwadhuru watu.
20 Watu wengine duniani hawakufa kwa mapigo haya. Lakini watu hawa bado hawakubadili mioyo yao na kuacha kuabudu vitu walivyovitengeneza kwa mikono yao wenyewe. Hawakuacha kuabudu mapepo na sanamu zilizotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, au kusikia au kutembea. 21 Hawakubadili mioyo yao na kuacha kuua watu wengine au kuacha uchawi, dhambi ya uzinzi na wizi.
© 2017 Bible League International