Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Sauti ya Tarumbeta ya Kwanza
6 Kisha malaika saba wenye tarumbeta walijiandaa kupuliza tarumbeta zao.
7 Malaika wa kwanza alipuliza tarumbeta yake. Mvua ya mawe na moto uliochanyanyikana na damu vilimwagwa chini duniani. Theluthi moja ya dunia na nyasi zote za kijani na theluthi ya miti vikaungua.
8 Malaika wa pili alipopuliza tarumbeta yake. Kitu fulani kilichoonekana kama mlima mkubwa unaowaka moto kilitupwa baharini. Na theluthi moja ya bahari ikawa damu. 9 Na theluthi moja ya viumbe walioumbwa wanaokaa baharini wakafa na ya meli theluthi moja zikaharibika.
10 Malaika wa tatu alipopuliza tarumbeta yake. Nyota kubwa, inayowaka kama tochi ikaanguka kutoka mbinguni. Ilianguka kwenye theluthi moja ya mito na chemichemi za maji. 11 Jina la nyota hiyo lilikuwa Uchungu.[a] Na theluthi moja ya maji yote yakawa machungu. Watu wengi wakafa kutokana na kunywa maji haya machungu.
12 Malaika wa nne alipopuliza tarumbeta yake. Theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota vikapigwa. Hivyo theluthi moja yao vikawa giza. Theluthi moja ya mchana na usiku ikakosa mwanga.
13 Nilipokuwa ninatazama, nilimsikia tai aliyekuwa anaruka juu sana angani akisema kwa sauti kuu, “Ole! Ole! Ole kwa wale wanaoishi duniani! Shida kuu zitaanza baada ya sauti za tarumbeta ambazo malaika wengine watatu watapuliza.”
Tarumbeta ya Tano Yaanzisha Kitisho cha Kwanza
9 Malaika wa tano alipopuliza tarumbeta yake, niliiona nyota ikianguka kutoka angani mpaka duniani. Nyota ilipewa ufunguo wa kufungulia shimo refu sana liendalo kuzimu. 2 Kisha nyota ikafungua shimo refu sana liendalo kuzimu. Moshi ukatoka kwenye shimo kama moto utokao kwenye tanuru kubwa. Jua na anga vikawa giza kwa sababu ya moshi uliotoka kwenye shimo.
3 Nzige wakatoka kwenye moshi na wakateremka kwenda duniani. Walipewa nguvu ya kuuma kama nge. 4 Waliamriwa kutoharibu nyasi au mimea ya mashambani na mti. Walitakiwa kuwadhuru watu wasio na alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao tu. 5 Hawakupewa mamlaka ya kuwaua lakini kuwatia maumivu kwa muda wa miezi mitano, maumivu kama ambayo mtu huyasikia anapoumwa na nge. 6 Siku hizo watu watatafuta kifo, lakini hawatakiona. Watataka kufa, lakini kifo kitajificha.
7 Nzige hao walionekana kama farasi walioandaliwa kwa ajili ya mapigano. Vichwani mwao walivaa kitu kilichoonekana kama taji ya dhahabu. Nyuso zao zilionekana kama nyuso za wanadamu. 8 Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake. Meno yao yalikuwa kama meno ya simba. 9 Vifua vyao vilionekana kama ngao za chuma. Sauti zilizotoka katika mbawa zao zilikuwa kama za farasi wengi na magari ya farasi yaendayo vitani. 10 Walikuwa na mikia kama ya nge. Nguvu ya kuwasababishia wanadamu maumivu kwa miezi mitano ilikuwa kwenye mikia yao. 11 Walikuwa na mtawala, aliyekuwa malaika wa kuzimu. Jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni.[b] Na kwa Kiyunani ni Apolioni.[c]
12 Kitisho cha kwanza kimepita sasa. Bado vinakuja vitisho vingine viwili.
© 2017 Bible League International