Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Barnaba na Sauli Wapewa Kazi Maalum
13 Walikuwepo baadhi ya manabii na walimu katika kanisa la Antiokia. Walikuwa Barnaba, Simeoni (ambaye pia aliitwa Nigeri[a]), Lukio (kutoka mji wa Kirene), Manaeni (aliyekua pamoja na Mfalme Herode[b]), na Sauli. 2 Watu hawa wote kwa pamoja walikuwa wanamwabudu Bwana na wamefunga Roho Mtakatifu alipowaambia, “Nitengeeni Barnaba na Sauli ili wanifanyie kazi maalumu. Wao ndio niliowachagua kuifanya kazi hiyo.”
3 Hivyo kanisa lilifunga na kuomba. Wakaweka mikono yao juu ya Barnaba na Sauli, wakaagana nao na kuwaacha waende.
Barnaba na Sauli Wakiwa Kipro
4 Barnaba na Sauli walitumwa na Roho Mtakatifu. Walikwenda katika mji wa Seleukia. Kutoka hapo walitweka tanga na kusafiri mpaka kwenye kisiwa cha Kipro. 5 Barnaba na Sauli walipofika kwenye mji wa Salami, walihubiri ujumbe wa Mungu katika masinagogi ya Kiyahudi. Yohana ambaye pia anaitwa Marko alikuwa pamoja nao ili kuwasaidia.
6 Walisafiri wakitisha kisiwa chote mpaka kwenye mji wa Pafo. Huko walimkuta mwanaume wa Kiyahudi aliyeitwa Bar-Yesu aliyekuwa akifanya uchawi. Alikuwa nabii wa uongo. 7 Alikaa daima karibu na Sergio Paulo, aliyekuwa gavana na mtu makini sana. Sergio Paulo aliwaalika Barnaba na Sauli waende kumtembelea kwa sababu alitaka kusikia ujumbe wa Mungu. 8 Lakini mchawi Elima (Bar-Yesu kama alivyoitwa kwa Kiyunani) alizungumza kinyume nao ili kuwapinga, akijaribu kumzuia gavana asimwamini Yesu. 9 Kisha Sauli (ambaye pia anajulikana kama Paulo), akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkazia macho Elima 10 na kusema, “Ewe mwana wa Ibilisi, uliyejaa uongo na aina zote za hila za uovu! Wewe ni adui wa kila kilicho cha kweli. Hautaacha kuzibadili kweli za Bwana kuwa uongo? 11 Sasa Bwana atakugusa na utakuwa asiyeona. Hautaweza kuona kitu chochote kwa muda, hata mwanga wa jua.”
Ndipo kila kitu kikawa giza kwa Elima. Akazunguka kila mahali na akapotea. Alikwenda kila mahali akijaribu kumpata mtu wa kumshika mkono ili amwongoze. 12 Gavana alipoyaona haya, akaamini. Akayashangaa mafundisho kuhusu Bwana.
© 2017 Bible League International