Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
9 Ndugu zangu, ninajua kuwa mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi kwa bidii. Tulifanya kazi usiku na mchana ili tujitegemee, pasipo kumwelemea mtu yeyote wakati tukifanya kazi ya kuhubiri Habari Njema za Mungu.
10 Tulipokuwa pamoja nanyi enyi mnaoamimi, tulikuwa safi, wa kweli, na wasio na kosa lolote kwa namna tulivyoishi maisha matakatifu. Mnafahamu, kama vile Mungu anavyotenda, kuwa jambo hili ni la kweli. 11 Mnafahamu jinsi tulivyo mtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea wanaye. 12 Tuliwatia moyo, tuliwafariji, na tuliwaambia kuishi maisha mema kwa Mungu. Yeye anawaita muwe sehemu ya maisha mema mbele za Mungu.
13 Pia, tunamshukuru Mungu pasipo kuacha kwa sababu ya namna mlivyoupokea ujumbe wake. Ingawa tuliuleta kwenu, mliupokea si kama ujumbe unaotoka kwa wanadamu, bali kama ujumbe wa Mungu. Kweli hakika ni ujumbe kutoka kwa Mungu, unaofanya kazi kwenu ninyi mnao uamini.
Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini
(Mk 12:38-40; Lk 11:37-52; 20:45-47)
23 Kisha Yesu akazungumza na watu pamoja na wafuasi wake, akasema, 2 “Walimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kuwaambia Sheria ya Musa inasema nini. 3 Hivyo mnapaswa kuwatii. Fanyeni kila wanachowaambia. Lakini maisha yao sio mfano mzuri wa kuufuata. Hawatendi wale wanayofundisha. 4 Hutengeneza orodha ndefu ya kanuni na kujaribu kuwalazimisha watu kuzifuata. Lakini sheria hizi ni kama mizigo mizito ambayo watu hawawezi kuibeba, na viongozi hawa hawatazirahisisha kupunguza mzigo kwa watu.
5 Wao wanatenda mambo mema tu ili waonwe na watu wengine. Hufanya visanduku vidogo vya Maandiko[a] wanavyovaa kuwa vikubwa zaidi. Hufanya mashada ya urembo[b] kwenye mavazi yao ya nje kuwa marefu zaidi ili waonwe na watu. 6 Watu hawa wanapenda kukaa sehemu za heshima kwenye sherehe na kwenye viti muhimu zaidi katika masinagogi. 7 Wanapenda kuitwa ‘Mwalimu’ Na kusalimiwa kwa heshima na watu kwenye masoko.
8 Ninyi nyote ni ndugu, dada na kaka kwa sababu mnaye mwalimu mmoja tu. Hivyo msikubali kuitwa ‘Mwalimu’. 9 Nanyi msimwite mtu yeyote duniani ‘Baba’, maana mnaye Baba mmoja tu, naye yuko mbinguni. 10 Msikubali kuitwa ‘Mwalimu’, kwa sababu mnaye Mwalimu mmoja tu, naye ni Masihi. 11 Kila atakayetumika kama mtumishi ndiyo mkuu zaidi kati yenu. 12 Wanaojifanya kuwa bora kuliko wengine watanyenyekezwa kwa lazima. Lakini watu wanaojinyenyekeza wenyewe watafanywa kuwa wakuu.
© 2017 Bible League International