Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mk 9:30-32; Lk 9:43b-45)
22 Baadaye, wafuasi walipokusanyika pamoja Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwenye mamlaka ya watu wengine, 23 watakaomwua. Lakini atafufuliwa kutoka kwa wafu siku ya tatu.” Wafuasi waliposikia kuwa Yesu angeuawa walihuzunika sana.
Yesu Afundisha Kuhusu Kulipa Kodi
24 Yesu na wafuasi wake walikwenda Kapernaumu. Walipofika huko watu waliokuwa wakikusanya ushuru wa Hekalu[a] wakamwendea Petro na kumwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa kodi ya Hekalu?”
25 Petro akajibu, “Ndiyo, hulipa.”
Petro akaingia katika nyumba alimokuwa Yesu. Kabla Petro hajazungumza jambo lolote, Yesu akamwambia, “Wafalme wa dunia huchukua kila aina ya kodi kutoka kwa watu. Lakini ni akina nani ambao hutoa kodi? Je, ni jamaa wa familia ya mfalme? Au watu wengine ndiyo hulipa kodi? Unadhani ni akina nani?”
26 Petro akajibu, “Watu wengine ndiyo hulipa kodi.”
Yesu akasema, “Basi wana wa mfalme hawapaswi kulipa kodi. 27 Lakini kwa kuwa hatutaki kuwaudhi watoza ushuru hawa, basi fanya hivi: Nenda ziwani na uvue samaki. Utakapomkamata samaki wa kwanza, mfungue kinywa chake. Ndani ya kinywa chake utaona sarafu nne za drakma mdomoni mwake. Ichukue sarafu hiyo mpe mtoza ushuru. Hiyo itakuwa kodi kwa ajili yangu mimi na wewe.”
© 2017 Bible League International