Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Maagizo ya Mwisho
4 Kaka na dada zangu wapenzi, ninawapenda na ninataka kuwaona. Mnanifurahisha na ninajivuna kwa sababu yenu. Endeleeni kuwa imara kumfuata Bwana kama nilivyowaambia.
2 Ninawasihi Euodia na Sintike, ninyi nyote wawili ni wa Bwana, hivyo muwe na mtazamo mmoja. 3 Kwa ajili ya hili ninamwomba rafiki yangu aliyetumika pamoja nami kwa uaminifu: Wasaidieni wanawake hawa. Waliwahubiri watu Habari Njema kwa bidii kama watendaji wenzangu tukiwa pamoja na Klementi na wengine waliofanya kazi pamoja nami. Majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.[a]
4 Furahini katika Bwana daima. Ninasema tena, furahini.
5 Kila mtu auone wema na uvumilivu wenu. Bwana yu karibu kuja. 6 Msisumbuke kitu chochote, lakini salini na kumwomba Mungu kwa mahitaji yenu. Mshukuruni Mungu wakati mnapomwomba yale mnayohitaji. 7 Na kwa kuwa ninyi ni milki ya Kristo Yesu, amani ya Mungu itailinda mioyo na mawazo yenu isipate wasiwasi. Amani yake inaweza kutenda haya zaidi ya akili za kibinadamu.[b]
8 Na sasa, mwisho kabisa, kaka na dada zangu, fikirini kuhusu yale yaliyo ya kweli, ya kuheshimiwa, ya haki, yaliyo safi, yenye kupendeza, na yanayosemwa vema. 9 Yatendeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu, niliyowaambia na yale mliyoyaona nikitenda. Na Mungu atoaye amani atakuwa pamoja nanyi.
Simulizi Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Sherehe
(Lk 14:15-24)
22 Yesu aliendelea kuwajibu viongozi wa Kiyahudi kwa mifano zaidi. Akasema, 2 “Ufalme wa Mungu unafanana na jambo lililotokea mfalme alipoandaa sherehe ya harusi kwa ajili ya mwanaye. 3 Aliwaalika baadhi ya watu. Wakati ulipofika mfalme aliwatuma watumwa wake kuwaambia watu waende kwenye sherehe. Lakini walikataa kwenda kwenye sherehe ya mfalme.
4 Ndipo mfalme aliwaita baadhi ya watumishi wengine zaidi na akawaambia namna ya kuwaambia wale aliowaalika: ‘Njooni sasa! Sherehe imeandaliwa. Nimechinja ng'ombe wangu madume na ndama wanono waliolishwa nafaka, na kila kitu kiko tayari kuliwa. Njooni kwenye sherehe ya harusi.’
5 Lakini watu walioalikwa hawakujali yale waliyoambiwa na watumwa wa mfalme. Wengine waliondoka wakaenda kufanya mambo mengine. Mmoja alikwenda shambani na mwingine alikwenda kwenye shughuli zake. 6 Wengine waliwakamata watumwa wa mfalme, wakawapiga na kuwaua. 7 Mfalme alikasirika sana na akatuma jeshi lake kuwaua wale waliowaua watumwa wake. Na jeshi likauchoma moto mji wao.
8 Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Sherehe ya harusi iko tayari. Niliwaalika wale watu lakini hawakustahili. 9 Hivyo nendeni kwenye pembe za mitaa na mwalikeni kila mtu mtakayemwona, waambieni waje kwenye sherehe yangu.’ 10 Hivyo watumwa wake waliingia mitaani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wabaya na wema na kuwaleta kwenye sherehe. Na jumba la sherehe likawa na wageni wengi.
11 Mfalme alipoingia ili kuwasalimu wageni, alimwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi rasmi la harusi. 12 Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki ilikuwaje ukaruhusiwa kuingia humo? Hujavaa vazi nadhifu kwa arusi!’ Lakini mtu yule hakuwa na neno la kusema. 13 Hivyo mfalme akawaambia baadhi ya wale waliokuwa wanawahudumia watu kwa chakula, ‘Mfungeni mtu huyu mikono na miguu yake na mtupeni gizani, ambako watu wanalia na kusaga meno yao kwa maumivu.’
14 Ndiyo, watu wengi wamealikwa, lakini wachache tu ndiyo waliochaguliwa.”
© 2017 Bible League International