Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo Anayo Mambo ya Mwisho ya Kusema
16 Napenda mjue kuwa mnaweza kumwamini dada yetu Foebe. Ni mtumishi maalum wa kanisa la kule Kenkrea. 2 Nawaomba mmkaribishe kama yule aliye wa Bwana. Mkaribisheni kwa jinsi ambayo watu wa Mungu wanapaswa. Msaidieni kwa chochote atakachohitaji kutoka kwenu. Yeye amekuwa kiongozi anayeheshimika ambaye amewasaidia watu wengine wengi, pamoja na mimi.
3 Mpeni salamu Priska na Akila, ambao wametumika pamoja nami kwa ajili ya Kristo Yesu. 4 Waliyahatarisha maisha yao wenyewe ili wayaokoe maisha yangu. Nawashukuru hao, na makanisa yote ya wasio Wayahudi yanawashukuru wao.
5 Vilevile, fikisheni salamu katika kanisa linalokusanyikia nyumbani mwao.
Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto. Alikuwa mtu wa kwanza kumfuata Kristo kule Asia. 6 Pia msalimieni Mariamu ambaye alifanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili yenu. 7 Pia msalimieni Androniko na Yunia. Hao ni jamaa zangu, na walikuwa gerezani pamoja nami. Walikuwa wafuasi wa Kristo kabla yangu. Nao ni miongoni mwa wale walio muhimu sana waliotumwa na Kristo kuifanya kazi yake.[a]
8 Msalimuni Ampliato, rafiki yangu mpendwa miongoni mwa watu wa Bwana, 9 na kwa Urbano. Aliyefanya kazi pamoja nasi kwa ajili ya Kristo. Pia fikisheni salamu kwa rafiki yangu mpendwa Stakisi
10 na Apele, aliyejithibitisha kuwa yeye ni mfuasi wa kweli wa Kristo.
Nisalimieni watu wote katika nyumba ya Aristobulo 11 na Herodioni, jamaa yangu.
Wasalimieni nyumba nzima ya Narkiso aliye wake Bwana 12 na Trifaina na Trifosa, wanawake wanaofanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili ya Bwana. Nisalimieni rafiki yangu mpendwa Persisi. Dada huyu amefanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili ya Bwana.
13 Pia msalimieni Rufo, mmoja wa wateule wa Bwana, na mama yake, ambaye amefanyika mama yangu pia.
14 Fikisheni salamu kwa Asinkrito, Flegoni, Hermesi, Patroba, Herma na waamini wote walio pamoja nao.
15 Msalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, Olimpa na watu wote wa Mungu walio pamoja nao.
16 Mpeni kila mmoja ile salamu maalum ya watu wa Mungu.[b]
Makanisa yote yaliyo ya Kristo yanatuma salamu zao kwenu.
© 2017 Bible League International