Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
14 Namsikia mtu akiuliza, “Hivyo hii ina maana gani? Je, Mungu si mwenye haki?” Hapana! 15 Mungu alimwambia Musa, “Nitampa rehema yeyote ninayetaka kumpa rehema. Nitamhurumia yeyote ninayemchagua.”(A) 16 Hivyo Mungu atamchagua yeyote anayeamua kumpa rehema pasipo kujali watu wanataka nini ama kwa jinsi gani wanapiga mbio. 17 Katika Maandiko Mungu anamwambia Farao: “Nilikuweka uwe mfalme kwa kusudi hili hasa: kuonesha nguvu zangu kupitia kwako. Nilitaka jina langu litangazwe ulimwenguni kote”(B) 18 Hivyo Mungu huwarehemu wale anaotaka kuwarehemu na huwafanya jeuri wale anaotaka wawe jeuri.
19 Hivyo utaniuliza, “Ikiwa unayosema ni kweli, kwa nini Mungu amlaumu mtu yeyote kwa kufanya makosa? Hayupo anayeweza kukataa kufanya yale anayotaka Mungu, Je, yupo?” 20 Hilo si la kuuliza. Wewe ni mwanadamu tu na huna haki ya kumhoji Mungu. Chungu hakiwezi kumhoji aliyekifinyanga. Hakiwezi kusema, “Kwa nini ulinifinyanga hivi?” 21 Yeye aliyefinyanga chungu anaweza kufinyanga kitu chochote anachotaka. Anautumia udongo ule ule wa mfinyanzi kufinyanga vitu mbalimbali. Anaweza kufinyanga kitu kimoja kwa makusudi maalumu na kingine kwa matumizi ya kila siku.
22 Ni kwa jinsi hiyo hiyo Mungu amefanya. Alitaka kuionesha hasira yake na kuwafanya watu waone nguvu zake. Lakini kwa uvumilivu wake aliwastahimili wale waliomuudhi, watu waliokuwa tayari kuangamizwa. 23 Alingoja kwa uvumilivu ili aweze kuutangaza utajiri wa utukufu wake kwa watu aliowachagua wapokee rehema zake. Mungu alikwisha waandaa kuushiriki utukufu wake. 24 Sisi ndiyo watu hao, ambao Mungu alituchagua si tu kutoka kwa Wayahudi lakini pia kutoka kwa wale wasio Wayahudi. 25 Kama Mungu anavyosema katika kitabu cha Hosea,
“Watu wasiokuwa wangu,
nitasema ni watu wangu.
Na watu ambao sikuwapenda,
nitasema ni watu ninaowapenda.(C)
26 Na pale Mungu aliposema zamani:
‘Ninyi si watu wangu’;
hapo wataitwa watoto wa Mungu aliye hai.”(D)
27 Na Isaya huililia Israeli:
“Wako watu wengi sana wa Israeli,
kuliko mchanga ulio pwani ya baharini.
Lakini wachache wao watakaookolewa.
28 Ndiyo, Bwana atakamilisha kwa haraka
aliyosema atayafanya duniani.”(E)
29 Ni kama vile alivyosema Isaya:
“Ikiwa Bwana Mwenye Uweza wote
asingewaruhusu watu wachache wakaishi,
tungekuwa tumeangamizwa kabisa,
kama vile miji miovu ya Sodoma, na Gomora.”(F)
© 2017 Bible League International