Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
37 Watu waliposikia hili wakahuzunika sana. Wakawauliza Petro na mitume wengine, “Ndugu zetu, tufanye nini?”
38 Petro akawaambia, “Geuzeni mioyo na maisha yenu na kila mmoja wenu abatizwe katika jina la Yesu Kristo. Ndipo Mungu atawasamehe dhambi zenu, na mtapokea zawadi ya Roho Mtakatifu. 39 Ahadi hii ni kwa ajili yenu ninyi, watoto wenu na vizazi vijavyo. Ni kwa kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu anamwita kwake mwenyewe.”
40 Petro aliwaonya kwa maneno mengine mengi; aliwasihi, akawaambia, “Jiokoeni na uovu unaofanywa na watu wanaoishi sasa!” 41 Ndipo wale walioyakubali yale aliyosema Petro wakabatizwa. Yapata watu elfu tatu waliongezwa kwenye kundi la waamini siku ile.
Ushirika wa Waamini
42 Waamini walitumia muda wao kusikiliza mafundisho ya mitume. Walishirikiana kila kitu kwa pamoja. Walikula[a] na kuomba pamoja. 43 Maajabu mengi na ishara nyingi zilikuwa zinatokea kupitia mitume, na hivyo kila mtu aliingiwa na hofu na akamtukuza Mungu. 44 Waamini wote walikaa pamoja, na kushirikiana kila kitu. 45 Waliuza mashamba yao na vitu walivyomiliki, kisha wakatoa fedha na kuwapa wenye kuhitaji. 46 Waamini waliendelea kukutana pamoja katika eneo la Hekalu. Pia walikula pamoja katika nyumba zao. Walikuwa na furaha kushirikiana chakula chao na walikula kwa mioyo mikunjufu. 47 Waamini walimsifu Mungu na waliheshimiwa na watu wote. Watu wengi zaidi waliokolewa kila siku, na Bwana alikuwa akiwaongeza kwenye kundi lao.
© 2017 Bible League International