Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Dhambi na Sheria
7 Mnaweza kudhani ninasema ya kwamba dhambi na sheria vinafanana. Sisemi hivyo. Lakini sheria ilikuwa njia pekee ya kunifundisha maana ya dhambi. Nisingeweza kujua kwamba ni kosa kutamani kitu kisichokuwa changu. Lakini sheria inasema, “Usitamani mali ya mtu mwingine.”(A) 8 Na dhambi kwa kutumia amri hiyo, ikanifanya nitamani kila kitu kisichokuwa changu. Hivyo dhambi ilikuja kwangu kutokana na amri hiyo. Lakini bila sheria, dhambi imekufa na haina nguvu. 9 Kabla sijaijua sheria, nilikuwa hai. Lakini nilipoijua sheria, dhambi ikaanza kuishi ndani yangu, 10 na hiyo ikawa na maana ya kifo kwangu. Amri ilikusudiwa kuleta uzima, lakini kwangu iliniletea kifo. 11 Dhambi ilipata njia ya kunidanganya kwa kutumia amri ili nife.
12 Hivyo, sheria ni takatifu na amri ni takatifu, sahihi na nzuri. 13 Je, hii ina maana kuwa kitu ambacho ni kizuri kiliniletea kifo? Hapana, ni dhambi iliyoitumia amri nzuri ndiyo iliyoniletea kifo. Hii inaonesha kwa hakika kuwa dhambi ni dhambi. Dhambi inaweza kutumia amri iliyo nzuri na kuleta matokeo yanayoonesha ubaya wake mkubwa.
Vita ndani Yetu
14 Tunafahamu kuwa sheria ni ya rohoni, lakini mimi si wa rohoni. Mimi ni mwanadamu hasa. Dhambi inanitawala kana kwamba mimi ni mtumwa wake. 15 Sielewi ni kwa nini ninatenda jinsi ninavyotenda. Sitendi mema ninayotaka kuyatenda, bali ninatenda maovu ninayoyachukia. 16 Na ikiwa ninatenda kile nisichotaka kutenda, inamaanisha kuwa ninakubali kuwa sheria ni njema. 17 Lakini kwa hakika siyo mimi mwenyewe ninayetenda maovu. Bali dhambi inayokaa ndani yangu ndiyo inatenda hayo. 18 Ndiyo, ninajua kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu, nina maana kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu kisichokuwa cha rohoni. 19 Sitendi mema ninayotaka nitende. Ninatenda maovu nisiyotaka kutenda. 20 Hivyo ikiwa ninatenda yale nisiyotaka kutenda, hakika si mimi ninayeyatenda hayo. Bali dhambi inayoishi ndani yangu ndiyo inayotenda.
© 2017 Bible League International