Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
55 Lakini Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama juu mbinguni, na kuuona utukufu wa Mungu. Alimwona Yesu amesimama upande wa kulia wa Mungu. 56 Stefano akasema, “Tazama! Naona mbingu zimefunguka. Na ninamwona Mwana wa Adamu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”
57 Kila mmoja pale akaanza kupiga kelele, wakaziba masikio yao kwa mikono yao. Wote kwa pamoja wakamvamia Stefano. 58 Wakamtoa nje ya mji na kuanza kumpiga kwa mawe. Mashahidi walioshuhudia uongo kinyume cha Stefano waliacha makoti yao kwa kijana aliyeitwa Sauli. 59 Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa.
2 Kama watoto wachanga, mnapaswa kuyatamani maziwa ya kiroho yaliyo safi, ili kwa ajili ya hayo muweze kukua na kuokolewa, 3 kwa vile mmekwisha kuujaribu wema wa Bwana.
4 Mkaribieni Bwana Yesu, aliye Jiwe lililo Hai, lililokataliwa na watu, bali kwa Mungu ni jiwe lililoteuliwa na kuheshimika. 5 Ninyi pia, kama mawe yaliyo hai mnajengwa ili kuwa hekalu la kiroho. Mmekuwa makuhani watakatifu mkimtumikia Mungu kwa kutoa sadaka za kiroho zinazokubalika kwake kwa njia ya Yesu Kristo. 6 Hivyo, Maandiko yanasema,
“Tazameni, naweka katika Sayuni Jiwe la msingi katika jengo,
lililoteuliwa na kuheshimika,
na yeyote anayeamini hataaibishwa.”(A)
7 Inamaanisha heshima kwenu mnaoamini, bali kwa wasioamini,
“jiwe walilolikataa wajenzi
limekuwa jiwe la muhimu kuliko yote.”(B)
8 Na,
“jiwe linalowafanya watu wajikwae
na mwamba unaowafanya watu waanguke.”(C)
Walijikwaa kwa sababu hawakuutii ujumbe wa Mungu, na Mungu alisema hilo litatokea wasipotii.
9 Lakini ninyi ni watu mlioteuliwa, ni Ukuhani unaomtumikia Mfalme. Ninyi ni taifa takatifu nanyi ni watu wa Mungu. Yeye aliwaita Ili muweze kutangaza matendo yake yenye nguvu. Naye aliwaita mtoke gizani na mwingie katika nuru yake ya ajabu.
10 Kuna wakati hamkuwa watu,
lakini sasa mmekuwa watu wa Mungu.
Kuna wakati hamkuoneshwa rehema,
lakini sasa mmeoneshwa rehema za Mungu.
Yesu Awafariji Wafuasi Wake
14 Yesu akasema, “Msisumbuke. Mwaminini Mungu, na mniamini na mimi. 2 Kuna vyumba vya kutosha katika nyumba ya Baba yangu. Nisingewaambia hivi ikiwa isingelikuwa kweli. Ninaenda huko kuandaa mahali kwa ajili yenu. 3 Nitakapomaliza kuandaa, nitarudi. Kisha nitawachukua ili muwe pamoja nami mahali niliko. 4 Mnaijua njia iendayo kule ninakokwenda.”
5 Thomaso akasema, “Bwana, hatujui unakokwenda, sasa tutaijuaje njia?”
6 Yesu akajibu, “Mimi ndiye njia, kweli, na uzima. Njia pekee ya kwenda kwa Baba ni kupitia kwangu. 7 Kwa kuwa sasa ninyi nyote mmenijua, mtamjua Baba yangu pia. Kwa kweli, sasa mnamjua Baba na mmekwisha kumwona.”
8 Filipo akamwambia, “Bwana, utuonyeshe Baba. Hilo tu ndilo tunalohitaji.”
9 Yesu akajibu, “Nimekuwa pamoja nanyi kwa kipindi kirefu. Hivyo wewe, Filipo unapaswa kunijua. Yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba pia. Hivyo kwa nini unasema, ‘Utuonyeshe Baba’? 10 Hamwamini kuwa mimi nimo ndani ya Baba na Baba naye yumo ndani yangu? Mambo niliyowaambia hayatoki kwangu. Baba anakaa ndani yangu, naye anafanya kazi yake mwenyewe. 11 Mniamini ninaposema kwamba nimo ndani ya Baba na Baba yumo ndani yangu. Vinginevyo muamini kwa sababu ya miujiza niliyoifanya.
12 Hakika nawaambia, yeyote anayeniamini atafanya mambo kama yale niliyoyafanya. Naye atafanya mambo makubwa zaidi ya yale niliyofanya, kwa sababu mimi naenda kwa Baba. 13 Na kama mtaomba jambo lo lote kwa jina langu, nitawafanyia. Kisha utukufu wa Baba utadhihirishwa kupitia kwa Mwana wake. 14 Ikiwa mtaniomba chochote kwa jina langu, mimi nitakifanya.
© 2017 Bible League International