Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mfano wa Ibrahimu
4 Basi tuseme nini kuhusu Ibrahimu,[a] baba wa watu wetu? 2 Ikiwa Ibrahimu alifanywa kuwa mwenye haki kutokana na matendo yake, hicho ni kitu cha kujivunia! Lakini kama Mungu aonavyo, hakuwa na sababu ya kujivuna. 3 Hili ni wazi kama Maandiko yanavyosema, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa sababu ya kuamini kwake, Mungu alimhesabu kuwa mwenye haki.”[b]
4 Watu wanapofanya kazi, mshahara wao hautolewi kama zawadi. Ni kitu wanachopata kutokana na kazi waliyofanya. 5 Lakini watu hawawezi kufanya kazi yoyote itakayowafanya wahesabiwe kuwa wenye haki mbele za Mungu. Hivyo ni lazima wamtumaini Yeye. Kisha huikubali imani yao na kuwahesabia haki. Yeye ndiye anayewahesabia haki hata waovu.
Ahadi ya Mungu Hupokelewa kwa Imani
13 Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu na wazaliwa wake ya kuwapa ulimwengu wote. Lakini kwa nini Mungu aliweka ahadi hii? Haikuwa kwa sababu Ibrahimu aliifuata sheria. Ni kwa sababu aliiweka imani yake katika Mungu na akakubaliwa kuwa mwenye haki. 14 Watu wa Mungu watarithi yote ambayo Mungu alimwahidi Ibrahimu, lakini si kwa sababu wanaifuata sheria. Ikiwa ni lazima tuitii sheria ili tupate kile alichoahidi Mungu, badi imani ya Ibrahimu haina maana yoyote na ahadi ya Mungu haina manufaa. 15 Ninasema hivi kwa sababu sheria ndiyo huleta hasira ya Mungu kwa wale wasioitii. Lakini ikiwa sheria haipo, basi hakuna hatia ya kutoitii.
16 Hivyo watu hupokea ahadi ya Mungu kwa imani. Hili hutokea ili ahadi hiyo iwe kipawa cha bure. Na ikiwa ahadi ni kipawa cha bure, basi watu wote wa Ibrahimu watapata ahadi hiyo. Ahadi hii si tu kwa ajili ya wale wanaoishi chini ya Sheria ya Musa. Bali ni kwa ajili ya wote wanaoishi kwa kuweka imani yao kwa Mungu kama Ibrahimu alivyofanya. Ni baba yetu sote. 17 Kama Maandiko yanavyosema, “Nimekufanya uwe baba wa mataifa mengi.”(A) Ibrahimu aliposikia ahadi hii, aliiweka imani yake kwa Mungu. Mungu ndiye awapaye uhai waliokufa na kwa amri yake huumba kisichokuwepo.
Yesu na Nikodemu
3 Alikuwepo mtu aliyeitwa Nikodemu, mmoja wa Mafarisayo. Yeye alikuwa kiongozi muhimu sana wa Kiyahudi. 2 Usiku mmoja alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa kutoka kwa Mungu. Hayupo mtu yeyote anayeweza kutenda ishara na miujiza unayotenda bila msaada wa Mungu.”
3 Yesu akajibu, “Hakika nakuambia, ni lazima kila mtu azaliwe upya.[a] Yeyote ambaye hajazaliwa mara ya pili hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.”
4 Nikodemu akasema, “Yawezekanaje mtu ambaye tayari ni mzee akazaliwa tena? Je, anaweza kuingia tena katika tumbo la mama yake na kuzaliwa kwa mara ya pili?”
5 Yesu akamjibu, “Uniamini ninapokwambia kuwa kila mtu anapaswa kuzaliwa tena kwa maji na kwa Roho. Yeyote ambaye hakuzaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. 6 Maisha pekee ambayo watu huyapata kutoka kwa wazazi wao ni ya kimwili. Lakini maisha mapya anayopewa mtu na Roho ni ya kiroho. 7 Usishangae kwa kuwa nilikuambia, ‘Ni lazima mzaliwe upya.’ 8 Upepo huvuma kuelekea popote unakopenda. Unausikia, lakini huwezi kujua unakotoka na unakoelekea. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kila aliyezaliwa kwa Roho.”
9 Nikodemu akauliza, “Je, haya yote yanawezekana namna gani?”
10 Yesu akasema, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Israeli, inakuwaje huelewi mambo haya? 11 Ukweli ni kwamba, tunaongea yale tunayoyafahamu. Tunayasema yale tuliyoyaona. Hata hivyo ninyi hamyakubali yale tunayowaambia. 12 Nimewaeleza juu ya mambo ya hapa duniani, lakini hamniamini. Vivyo hivyo nina uhakika hamtaniamini hata nikiwaeleza mambo ya mbinguni! 13 Sikiliza, hakuna mtu aliyewahi kwenda kwa Mungu mbinguni isipokuwa Mwana wa Adamu. Yeye pekee ndiye aliyekuja duniani kutoka mbinguni.”
14 Unakumbuka yule nyoka wa shaba ambaye Musa alimwinua kule jangwani?[b] Vivyo hivyo Mwana wa Adamu anapaswa kuinuliwa juu. 15 Kisha kila anayemwamini aweze kuupata uzima wa milele.[c]
16 Kweli, hivi ndivyo Mungu alivyouonyesha upendo wake mkuu kwa ulimwengu: akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu anayemwamini asiharibiwe na mauti bali aupate uzima wa milele. 17 Mungu alimtuma Mwanawe ili kuuokoa ulimwengu. Hakumtuma kuja kuuhukumu na kuuweka hatiani, bali kuuokoa kwa njia ya mwanawe.
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mk 9:2-13; Lk 9:28-36)
17 Siku sita baadaye, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo na akapanda nao kwenye mlima mrefu. Walikuwa peke yao huko. 2 Wafuasi wake hawa walipokuwa wakimwangalia, Yesu alibadilika. Uso wake ukawa angavu kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama mwanga. 3 Ndipo wanaume wawili waliozungumza naye wakaonekana wakiwa pamoja naye. Walikuwa Musa na Eliya.
4 Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tuko hapa. Ukitaka, nitajenga vibanda vitatu,[a] kimoja kwa ajili ya heshima yako, kingine kwa ajili ya heshima ya Musa na kingine kwa ajili ya heshima ya Eliya.”
5 Petro alipokuwa akizungumza, wingu jeupe liliwafunika. Sauti ikatoka katika wingu na akasema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda, ninafurahishwa naye. Mtiini yeye!”
6 Wafuasi waliokuwa na Yesu walipoisikia sauti hii waliogopa sana na wakaanguka chini. 7 Lakini Yesu akawaendea na kuwagusa. Akasema, “simameni, msiogope.” 8 Wafuasi wakatazama juu, wakaona kuwa Yesu yuko peke yake.
9 Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, akawaamuru akisema: “Msimwambie mtu yeyote yale mliyoyaona mlimani. Subirini mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu. Ndipo mtaweza kuwaambia watu juu ya kile mlichokiona.”
© 2017 Bible League International