Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Yesu Alituagiza Kuwapenda Wengine
7 Wapendwa rafiki zangu, siwaandiki ninyi amri mpya. Ni amri ile ile ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ni fundisho lile lile ambalo mmekwishalisikia. 8 Lakini kile ninachokiandika pia ni amri mpya. Ni kweli; Mnaweza kuiona kweli ndani ya Yesu na ndani yenu ninyi wenyewe. Giza linatoweka, na nuru ya kweli tayari inang'aa.
9 Mtu anaweza kusema, “Niko nuruni,” lakini ikiwa anamchukia ndugu yeyote katika familia ya Mungu, basi angali bado katika giza. 10 Wao wanaowapenda ndugu wanaishi katika nuru, na hakuna kitu ndani yao cha kuwafanya watende mabaya. 11 Lakini yeyote anayemchukia nduguye wa kike au wa kiume yuko gizani. Anaishi katika giza. Hajui anakoenda, kwa sababu giza limemfanya asiweze kuona.
12 Ninawaandikia, ninyi watoto wapendwa,
kwa sababu dhambi zenu zimesamehewa kwa njia ya Kristo.
13 Ninawaandikia, ninyi akina baba,
kwa sababu mnamjua yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia, ninyi vijana,
kwa sababu mmemshinda yule mwovu.
14 Ninawaandikia ninyi watoto,
kwa sababu mnamjua Baba.
Ninawaandikia ninyi, akina baba,
kwa sababu mnamfahamu yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia ninyi, vijana,
kwa sababu mna nguvu.
Mafundisho ya Neno la Mungu yimo ndani yenu,
na mmemshinda yule mwovu.
15 Msiipende dunia hii ya uovu wala mambo yaliyomo ndani yake. Kama mkiipenda dunia, upendo wa baba haumo ndani yenu. 16 Yote yaliyomo katika dunia: yaani, tamaa halisi za kibinadamu, tamaa kwa yale mabaya tunayoyaona, na kiburi cha vitu tulivyonavyo. Lakini hakuna hata mojawapo ya haya litokalo kwa Baba. Yote yanatoka katika dunia. 17 Dunia inapita, na mambo yote ambayo watu wanayataka kutoka katika dunia nayo yanapita. Lakini yeyote atendaye mambo ambayo Mungu anayataka ataishi milele.
© 2017 Bible League International