Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mitume Wengine Wamkubali Paulo
2 Baada ya miaka 14 nilirudi tena Yerusalemu nikiwa na Barnaba na nilimchukua Tito pia. 2 Nilikwenda kule maana Mungu alinionyesha kuwa ninapaswa kwenda. Niliwafafanulia Habari Njema kama nilivyoihubiri kwa watu wasio Wayahudi. Pia nilikutana faragha na wale waliokuwa wanatazamiwa kuwa viongozi. Nilitaka niwe na uhakika kuwa tulikuwa tunapatana ili kazi yangu ya nyuma na ile niliyokuwa naifanya sasa zisipotee bure.
3 Tito, aliyekuwa pamoja nami ni Myunani. Hata hivyo viongozi hawa hawakulazimisha kumtahiri. 4 Tulihitaji kuyazungumzia matatizo haya, kwa sababu wale waliojifanya kuwa ni ndugu zetu walikuja kwenye kundi letu kwa siri. Waliingia kama wapelelezi kutafiti kuhusu uhuru tuliokuwa nao ndani ya Kristo Yesu. Walitaka watufanye sisi watumwa, 5 lakini hatukujiweka chini ya chochote ambacho hawa ndugu wa uongo walikitaka. Tulitaka ukweli wa Habari Njema ubaki ule ule na hatimaye uwafikie na ninyi.
6 Na watu wale ambao walihesabiwa kuwa viongozi muhimu hawakuongeza lolote katika ujumbe wa Habari Njema niliyowahubiria watu. (Haijalishi kwangu kuwa walikuwa wa “muhimu” au la. Kwa Mungu binadamu wote ni sawa.) 7 Lakini viongozi hawa waliona kuwa Mungu alinipa kazi maalumu ya kuhubiri Habari Njema kwa wasio Wayahudi, kama vile alivyomwagiza Petro[a] kufanya kazi hiyo hiyo ya kuhubiri Habari Njema miongoni mwa Wayahudi. 8 Mungu alimpa Petro uwezo wa kufanya kazi kama mtume lakini kwa walio Wayahudi. Mungu akanipa mimi pia uwezo wa kufanya kazi kama mtume, lakini kwa wasiokuwa Wayahudi. 9 Yakobo, Petro na Yohana walikuwa viongozi muhimu kanisani. Hawa wakaona kuwa Mungu alinipa kipaji hiki maalumu cha huduma, hivyo wakatupa mkono wa shirika mimi pamoja na Barnaba. Wakakubali kuwa sisi tutaendelea kufanya kazi miongoni mwao wasio Wayahudi, na wao wataendelea kufanya kazi miongoni mwao walio Wayahudi. 10 Wakatuomba jambo moja tu, ya kwamba tukumbuke kuwahudumia waaminio walio maskini.[b] Na kwa hakika hili lilikuwa jambo nililojitahidi kufanya.
© 2017 Bible League International