Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mamlaka ya Paulo ni Kutoka kwa Mungu
11 Ndugu zangu, ninawataka mjue kuwa ujumbe wa Habari Njema niliowaambia haukuandaliwa na mtu yeyote. 12 Sikuupata ujumbe wangu kutoka kwa mwanadamu yeyote. Habari Njema siyo kitu nilichojifunza kutoka kwa watu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia Habari Njema ninayowahubiri watu.
13 Mmesikia juu ya mwenendo wangu hapo zamani nilipokuwa mfuasi hodari wa dini ya Kiyahudi. Nililitesa kwa nguvu kanisa la Mungu, nikiwa na shabaha ya kuliangamiza kabisa. 14 Nilipata maendeleo makubwa katika dini ya Kiyahudi kwa kufanya kazi na kusoma kwa bidii kwa sababu nilikuwa mwaminifu kwa desturi za baba zetu.
15 Lakini Mungu alikuwa na mpango maalumu kwa ajili yangu hata kabla sijazaliwa.[a] Hivyo aliniita kwa neema yake. Na ilimpendeza 16 kumfunua Mwanaye ili niweze kuwahubiri Habari Njema watu wasio Wayahudi. Hicho ndicho nilichofanya baada ya hapo. Sikuomba ushauri ama msaada wowote kutoka kwa mtu yeyote. 17 Sikwenda Yerusalemu kuwaona wale waliokuwa mitume kabla mimi sijawa mtume. Badala yake, kwanza nilienda moja kwa moja Arabia. Kisha baadaye, nikarudi katika mji wa Dameski.
18 Miaka mitatu baadaye nilikwenda Yerusalemu kumwona Petro.[b] Nilikaa naye kwa siku 15. 19 Sikuonana na mtume mwingine yeyote, isipokuwa Yakobo mdogo wake Bwana peke yake. 20 Mungu anajua kuwa hakuna ninachowaandikia kisicho cha kweli. 21 Baadaye, nilielekea katika majimbo ya Shamu na Kilikia.
22 Lakini kwa wakati ule, makanisa ya Kristo yaliyokuwa Uyahudi yalikuwa bado hayajanifahamu mimi binafsi. 23 Walikuwa wamesikia tu juu yangu: “Mtu huyu alikuwa anatutesa. Lakini sasa anawaambia watu juu ya imani ile ile aliyojaribu kuiangamiza huko nyuma.” 24 Waamini hawa walimsifu Mungu kwa sababu yangu.
© 2017 Bible League International