Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Sauli Awa Mfuasi wa Yesu
9 Huko Yerusalemu Sauli aliendelea kuwatisha wafuasi wa Bwana, na hata kuwaambia kuwa angewaua. Alikwenda kwa kuhani mkuu, 2 na kumwomba aandike barua kwenda kwenye masinagogi yaliyokuwa katika mji wa Dameski. Sauli alitaka kuhani mkuu ampe mamlaka ya kuwatafuta watu katika mji wa Dameski waliokuwa wafuasi wa Njia ya Bwana.[a] Ikiwa angewapata waamini huko, wanaume au wanawake, angewakamata na kuwaleta Yerusalemu.
3 Hivyo Sauli alikwenda Dameski. Alipoukaribia mji, ghafla mwanga mkali kutoka mbinguni ukaangaza kumzunguka. 4 Akadondoka chini na akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa?”
5 Sauli akasema, “Wewe ni nani, Bwana?”
Sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu, unayemtesa. 6 Simama sasa na uingie mjini. Mtu mmoja huko atakueleza unachopaswa kufanya.”
7 Wanaume waliokuwa wanasafiri pamoja na Sauli walisimama pale kimya. Waliisikia sauti, lakini hawakumwona yeyote. 8 Sauli alisimama kutoka chini na kufumbua macho yake, lakini hakuweza kuona. Hivyo wale aliokuwa nao wakamshika mkono na kumwongoza kuingia Dameski. 9 Kwa siku tatu Sauli hakuweza kuona; hakula wala kunywa.
© 2017 Bible League International