Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
10 Nami kama mjenzi stadi nilijenga msingi wa nyumba hiyo kwa kutumia karama alizonipa Mungu. Wengine wanajenga pia katika msingi huo. Lakini kila mtu lazima awe mwangalifu kwa namna anavyojenga. 11 Yesu Kristo ndiye msingi uliokwishajengwa, na hakuna yeyote anayeweza kujenga msingi mwingine.
16 Hakika mnajua kuwa ninyi ni hekalu la Mungu na Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. 17 Ndiyo, ninyi nyote kwa pamoja ni Hekalu la Mungu. Na yeyote atakayeliharibu Hekalu la Mungu ataadhibiwa na Mungu, kwa sababu Hekalu la Mungu ni mali yake yeye mwenyewe.
18 Msijidanganye. Yeyote anayejiona kuwa ana hekima kwa viwango vya ulimwengu huu, basi na awe mpumbavu. Hiyo ndiyo njia pekee itakayomfanya kuwa na hekima. 19 Ninasema hivi kwa sababu hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu huwanasa katika mitego yao wenyewe wale wanaojidhania kuwa na hekima.”(A) 20 Pia Maandiko yanasema, “Bwana anajua mawazo ya wenye hekima. Anajua kuwa mawazo yao hayana maana.”(B) 21 Hivyo hakuna mtu yeyote duniani ambaye ninyi mnapaswa kujivunia. Kila kitu ni chenu: 22 Paulo, Apolo, Petro, ulimwengu, uzima, mauti, wakati uliopo na ujao, vyote hivi ni vyenu. 23 Ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.
Yesu Afundisha Kuhusu Kisasi
(Lk 6:29-30)
38 Mmesikia ilisemwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’(A) 39 Lakini ninawaambia msishindane na yeyote anayetaka kuwadhuru. Mtu akikupiga shavu la kulia mgeuzie na la kushoto pia. 40 Mtu akitaka kukushitaki ili akunyang'anye shati, mpe na koti pia. 41 Askari akikulazimisha kwenda naye maili moja,[a] nenda maili mbili pamoja naye. 42 Mpe kila anayekuomba, usimkatalie anayetaka kuazima kitu kwako.
Wapende Adui Zako
(Lk 6:27-28,32-36)
43 Mmesikia ilisemwa kuwa, ‘Wapende rafiki zako(B) na wachukie adui zako.’ 44 Lakini ninawaambia wapendeni adui zenu na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 45 Mkifanya hivi mtakuwa watoto halisi walio kama Baba yenu wa mbinguni. Yeye huwaangazia jua watu wote, bila kujali ikiwa ni wema au wabaya. Huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 Ikiwa mnawapenda wale wanaowapenda ninyi, kwa nini mpate thawabu toka kwa Mungu? Hata watoza ushuru hufanya hivyo. 47 Na ikiwa mnakuwa wema kwa rafiki zenu tu, ninyi si bora kuliko wengine. Hata watu wasiomjua Mungu ni wakarimu kwa rafiki zao pia. 48 Ninalosema ni kuwa, mkue hata kufikia upendo kamili[b] alionao baba yenu wa Mbinguni kwa watu wote.
© 2017 Bible League International