Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo Aeleza Kuhusu Kuokolewa Kwake
6 Lakini kitu fulani kilinitokea nikiwa njiani kwenda Dameski. Ilipokuwa inakaribia mchana na nilikuwa karibu na mji wa Dameski. Ghafla mwanga kutoka mbinguni ulining'aria kunizunguka. 7 Nilianguka chini na nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli kwa nini unanitesa?’
8 Niliuliza, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ Sauti ikasema, ‘Mimi ni Yesu kutoka Nazareti, unayemtesa.’ 9 Watu waliokuwa pamoja nami hawakuisikia sauti lakini waliona mwanga.
10 Nilisema, ‘Nifanye nini Bwana?’ Bwana alinijibu, ‘Simama na uingie Dameski. Humo utawaambia yote niliyopanga uyafanye.’ 11 Sikuweza kuona kwa sababu mwanga ule angavu ulinilemaza macho. Hivyo wale watu waliokuwa pamoja nami waliniongoza kuingia mjini Dameski.
12 Alikuwepo mtu mmoja katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania.[a] Mtu huyu alikuwa mcha Mungu na aliitii Sheria ya Musa na Wayahudi wote walioishi kule walimheshimu. 13 Alikuja kwangu na kuniambia, ‘Sauli, ndugu yangu, tazama juu na uone tena!’ Ghafla niliweza kumwona.
14 Anania aliniambia, ‘Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu alikuchagua wewe tangu zamani kuujua mpango wake. Amekuchagua wewe kumwona Mwenye Haki wake na kusikia maneno kutoka kwake. 15 Utakuwa shahidi wake kwa watu wote. Utawaambia ulichoona na kusikia. 16 Sasa usisubiri zaidi. Simama, ubatizwe na usafishwe dhambi zako, mwamini Yesu ili akuokoe.’[b]
17 Baadaye, nilirudi Yerusalemu. Nilipokuwa naomba katika eneo la hekalu, nikaona maono. 18 Nilimwona Yesu, naye akaniambia, ‘Haraka, ondoka Yerusalemu sasa hivi! Watu hapa hawataukubali ukweli unaowaambia kuhusu mimi.’
19 Nilisema, ‘Lakini, Bwana, Wayahudi wanajua kuwa mimi ndiye niliyewafunga gerezani na kuwapiga wale wanaokuamini wewe. Nilikwenda kwenye masinagogi yote kuwatafuta na kuwakamata Wayahudi wanaokuamini wewe. 20 Watu wanajua pia kuwa nilikuwepo wakati Stefano shahidi wako, alipouawa. Nilisimama pale na kukubaliana nao kuwa wamwue. Nilishikilia hata mavazi ya watu waliokuwa wanamwua!’
21 Lakini Yesu akaniambia, ‘Ondoka sasa. Nitakutuma mbali sana kwa watu wasio Wayahudi.’”
© 2017 Bible League International