Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Petro Amponya Kiwete
3 Siku moja Petro na Yohana walikwenda eneo la Hekalu saa tisa mchana, muda wa kusali na kuomba Hekaluni kama ilivyokuwa desturi. 2 Walipokuwa wanaingia katika eneo la Hekalu, mtu aliyekuwa mlemavu wa miguu maisha yake yote alikuwa amebebwa na baadhi ya rafiki zake waliokuwa wanamleta Hekaluni kila siku. Walimweka pembezoni mwa mojawapo ya Malango nje ya Hekalu. Lango hilo liliitwa Lango Zuri. Na mtu huyo alikuwa akiwaomba pesa watu waliokuwa wanaingia Hekaluni. 3 Siku hiyo alipowaona Petro na Yohana wakiingia eneo la Hekalu, aliwaomba pesa.
4 Petro na Yohana, walimtazama mtu huyo, wakamwambia, “Tutazame!” 5 Akawatazama akitumaini kuwa wangempa pesa. 6 Lakini Petro akasema, “Sina fedha wala dhahabu yoyote, lakini nina kitu kingine ninachoweza kukupa. Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama na utembee!”
7 Kisha Petro akamshika mkono wake wa kulia, akamnyenyua na kumsimamisha. Ndipo nyayo na vifundo vyake vikatiwa nguvu papo hapo. 8 Akaruka juu, akasimama kwa miguu yake na akaanza kutembea. Akaingia ndani ya eneo la Hekalu pamoja nao huku akitembea na kurukaruka akimsifu Mungu. 9-10 Watu wote walimtambua. Walimjua kuwa ni mlemavu wa miguu ambaye mara nyingi huketi kwenye Lango Zuri la Hekalu akiomba pesa. Lakini sasa walimwona anatembea na kumsifu Mungu. Walishangaa na hawakuelewa hili limewezekanaje.
© 2017 Bible League International