Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo na Barnaba Wakiwa Listra na Derbe
8 Katika mji wa Listra kulikuwa mtu aliyekuwa na tatizo katika mguu wake. Alizaliwa akiwa mlemavu wa miguu na hakuwahi kutembea. 9 Alikuwa amekaa akimsikiliza Paulo akizungumza. Paulo alipomwangalia kwa kumkazia macho alitambua kuwa mtu huyo alikuwa na imani kuwa Mungu angemponya. 10 Hivyo Paulo akapaza sauti na kumwambia, “Simama kwa miguu yako!” Mtu yule akaruka na kuanza kutembea.
11 Watu walipoona alichofanya Paulo, walipaza sauti kwa lugha yao wenyewe ya Kilikaonia. Walisema, “Miungu wamekuja kwetu katika maumbo ya kibinadamu!” 12 Watu wakaanza kumwita Barnaba “Zeusi”, na Paulo “Hermesi”, kwa sababu ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu. 13 Hekalu la Zeusi lilikuwa karibu na mji. Kuhani wa hekalu hili alileta mafahari ya ng'ombe kadhaa na mashada ya maua[a] kwenye lango la mji. Kuhani na watu walitaka kuwatolea sadaka Paulo na Barnaba.
14 Lakini mitume, Barnaba na Paulo walipoelewa jambo ambalo watu walikuwa wanafanya, walirarua mavazi yao.[b] Kisha wakakimbia kuingia katikati ya watu na kuwaambia kwa kupaza sauti zao wakisema: 15 “Ndugu, kwa nini mnafanya hivi? Sisi si miungu. Ni wanadamu kama ninyi. Tulikuja kuwaambia Habari Njema. Tunawaambia mviache vitu hivi visivyo na thamani. Mgeukieni Mungu wa kweli aishiye, aliyeumba mbingu, nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake.
16 Huko nyuma Mungu aliyaacha mataifa yote yatende yale waliyotaka. 17 Lakini daima Mungu alikuwepo na alitenda mambo mema yanayothibitisha kuwa yeye ni wa hakika na wa kweli. Huwapa mvua kutoka mbinguni na mavuno bora kwa wakati sahihi. Huwapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu kwa furaha.”
18 Hata baada Paulo na Barnaba kusema hayo, hawakuweza kuwazuia watu kuwatolea sadaka za kuteketezwa.
© 2017 Bible League International