Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
24 Mnajua kuwa katika riadha, wanariadha wengi hukimbia, lakini mmoja tu hupata zawadi. Hivyo kimbieni hivyo. Kimbieni ili mshinde! 25 Wote wanaoshiriki katika mchezo hufanya mazoezi kwa bidii ili waweze kushinda na kupata zawadi. Lakini zawadi wanazopata hazidumu milele. Lakini zawadi yetu ni ile inayodumu milele. 26 Hivyo ninakimbia kama mtu mwenye malengo. Ninapigana ngumi kama mpiganaji anayepiga kitu, si kama anayepiga hewa. 27 Ninaudhibiti mwili wangu kikamilifu na kuufanya unitiii kwa kila jambo ninalotaka kutenda. Ninafanya hivi ili mimi binafsi nisiikose thawabu baada ya kuwahubiri wengine Habari Njema.
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mt 8:1-4; Lk 5:12-16)
40 Ikatokea mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea Yesu na kupiga magoti hadi chini akimwomba msaada. Mtu huyo mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwambia Yesu, “Kama utataka, wewe una uwezo wa kuniponya nikawa safi.”
41 Aliposikia maneno hayo Yesu akakasirika.[a] Lakini akamhurumia. Akautoa mkono wake na kumgusa mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi, na kumwambia, “Ninataka kukuponya. Upone!” 42 Mara moja ugonjwa ule mbaya sana wa ngozi ulimwacha, naye akawa safi.
43 Baada ya hayo Yesu akampa maonyo yenye nguvu na kumruhusu aende zake mara moja. 44 Akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze,[b] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru[c] watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona kwa kuwa safi tena. Ukayafanye haya ili yawe uthibitisho kwa kila mmoja ya kwamba umeponywa.” 45 Lakini mtu yule aliondoka hapo na kwenda zake, na huko alianza kuzungumza kwa uhuru kamili na kusambaza habari hizo. Matokeo yake ni kwamba Yesu asingeweza tena kuingia katika mji kwa wazi wazi. Ikamlazimu kukaa mahali ambapo hakuna watu. Hata hivyo watu walikuja toka miji yote na kumwendea huko.
© 2017 Bible League International