Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Ahadi ya Mungu Hupokelewa kwa Imani
13 Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu na wazaliwa wake ya kuwapa ulimwengu wote. Lakini kwa nini Mungu aliweka ahadi hii? Haikuwa kwa sababu Ibrahimu aliifuata sheria. Ni kwa sababu aliiweka imani yake katika Mungu na akakubaliwa kuwa mwenye haki. 14 Watu wa Mungu watarithi yote ambayo Mungu alimwahidi Ibrahimu, lakini si kwa sababu wanaifuata sheria. Ikiwa ni lazima tuitii sheria ili tupate kile alichoahidi Mungu, badi imani ya Ibrahimu haina maana yoyote na ahadi ya Mungu haina manufaa. 15 Ninasema hivi kwa sababu sheria ndiyo huleta hasira ya Mungu kwa wale wasioitii. Lakini ikiwa sheria haipo, basi hakuna hatia ya kutoitii.
16 Hivyo watu hupokea ahadi ya Mungu kwa imani. Hili hutokea ili ahadi hiyo iwe kipawa cha bure. Na ikiwa ahadi ni kipawa cha bure, basi watu wote wa Ibrahimu watapata ahadi hiyo. Ahadi hii si tu kwa ajili ya wale wanaoishi chini ya Sheria ya Musa. Bali ni kwa ajili ya wote wanaoishi kwa kuweka imani yao kwa Mungu kama Ibrahimu alivyofanya. Ni baba yetu sote. 17 Kama Maandiko yanavyosema, “Nimekufanya uwe baba wa mataifa mengi.”(A) Ibrahimu aliposikia ahadi hii, aliiweka imani yake kwa Mungu. Mungu ndiye awapaye uhai waliokufa na kwa amri yake huumba kisichokuwepo.
18 Halikuwepo tumaini kwamba Ibrahimu angepata watoto, lakini alimwamini Mungu na akaendelea kutumaini. Na ndiyo sababu akafanyika kuwa baba wa mataifa mengi. Kama Mungu alivyomwambia kuwa, “Utakuwa na wazaliwa wengi.”(B) 19 Ibrahimu alikuwa na umri uliokaribia miaka 100, hivyo alikuwa amevuka umri wa kupata watoto. Pia, Sara hakuweza kuwa na watoto. Ibrahimu alilijua hili vizuri, lakini imani yake kwa Mungu haikudhoofika. 20 Hakutilia shaka kuwa Mungu angetenda kile alichoahidi. Hakuacha kuamini. Kwa hakika, aliendelea kuimarika katika imani yake. Alitukuza Mungu 21 na alikuwa na uhakika kuwa Mungu anaweza kutenda alichoahidi. 22 Ndiyo sababu “Mungu alimkubali kuwa ni mwenye haki”. 23 Maneno haya, “alikubaliwa”, yaliandikwa siyo tu kwa ajili ya Ibrahimu. 24 Pia yaliandikwa kwa ajili yetu. Mungu atatukubali sisi pia kwa sababu tunaamini. Tunamwamini yule aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 Yesu alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, na akafufuliwa kutoka kifo ili Mungu atuhesabie haki.
Mathayo Amfuata Yesu
(Mk 2:13-17; Lk 5:27-32)
9 Yesu alipokuwa anaondoka, alimwona mtu aliyeitwa Mathayo amekaa mahali pa kukusanyia ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Hivyo Mathayo akasimama na kumfuata Yesu.
10 Baadaye Yesu alikula chakula nyumbani kwa Mathayo. Watoza ushuru wengi na watu wenye sifa mbaya walikuja na kula chakula pamoja na Yesu pamoja na wafuasi wake. 11 Mafarisayo walipoona kuwa Yesu anakula pamoja na watu hao, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”
12 Yesu alipowasikia wakisema hili, akawaambia, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari si wenye afya. 13 Nendeni mkajifunze andiko hili linamaanisha nini: ‘Sihitaji dhabihu ya mnyama; Ninataka ninyi mwoneshe wema kwa watu.’(A) Sikuja kuwaalika wema kujiunga nami, bali wenye dhambi.”
Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa
(Mk 5:21-43; Lk 8:40-56)
18 Yesu alipokuwa bado anaongea, kiongozi wa sinagogi akamwendea. Kiongozi akainama chini mbele yake na akasema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini ikiwa utakuja na kumgusa kwa mkono wako, atafufuka.”
19 Hivyo Yesu na wafuasi wake wakaenda na mtu huyo.
20 Wakiwa njiani, alikuwepo mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili. Alimwendea Yesu kwa nyuma na akagusa sehemu ya chini ya vazi lake. 21 Aliwaza, “Ikiwa nitagusa tu joho lake, nitapona.”
22 Yesu aligeuka na kumwona mwanamke. Akasema, “Uwe na furaha, mwanamke. Imani yako imekuponya.” Kisha yule mwanamke akapona saa ile ile.
23 Yesu aliendelea kwenda na kiongozi wa Kiyahudi na kuingia nyumbani kwake. Aliwaona watu wapigao muziki kwa ajili ya mazishi pale. Na aliliona kundi la watu waliohuzunika sana. 24 Yesu akasema, “Ondokeni. Msichana hajafa. Amelala tu.” Lakini watu wakamcheka. 25 Baada ya watu kutolewa nje ya nyumba, Yesu aliingia kwenye chumba cha msichana. Aliushika mkono wa msichana na msichana akasimama. 26 Habari kuhusu jambo hili ilienea kila mahali katika eneo lile.
© 2017 Bible League International