Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
6 Ndugu zangu, nimemtumia Apolo na mimi mwenyewe kama mfano kwa ajili yenu. Nimefanya hivi ili mjifunze kutoka kwetu maana ya maneno yanayosema, “Uwe mwangalifu kufuata kilichoandikwa.”[a] 7 Kwa nini mnajisifu? Mlipewa kila kitu mlicho nacho. Sasa, ikiwa mlipewa kila kitu mlicho nacho, kwa nini mnajisifu kana kwamba mlipata vitu vyote kwa nguvu zenu wenyewe?
8 Mnadhani kwamba tayari mna kila kitu mnachohitaji. Mnadhani kwamba mmekwisha tajirika. Laiti mngekwisha fanywa wafalme, kwa sababu tungekuwa wafalme pamoja nanyi. 9 Lakini inaonekana kana kwamba Mungu amenipa mimi na mitume wengine mahali pa mwisho. Sisi ni kama wafungwa waliohukumiwa kufa, waliosimamishwa katika gwaride ili ulimwengu wote uwaone, si watu tu bali hata malaika pia. 10 Tu wapumbavu kwa kuwa sisi ni wa Kristo, lakini mnadhani kuwa ninyi ni wenye hekima katika Kristo. Sisi ni dhaifu, lakini mnadhani kuwa mna nguvu. Watu wanawaheshimu ninyi, na hawatuheshimu sisi. 11 Hata sasa hatuna vyakula vya kutosha kula au kunywa, na hatuna nguo za kutosha. Mara kwa mara tunapigwa na hatuna makazi. 12 Tunafanya kazi sana kwa mikono yetu ili tupate chakula. Watu wanapotutukana, tunamwomba Mungu awabariki. Watu wanapotutendea vibaya, tunavumilia. 13 Watu wanaposema mabaya juu yetu, tunawajibu kwa upole. Lakini watu wanaendelea kutuona kama takataka.
14 Siwaambii haya ili kuwatahayarisha, lakini ninaandika haya ili kuwaonya kama watoto wangu mwenyewe ninaowapenda. 15 Mnaweza kuwa na walimu elfu kumi katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Kupitia Habari Njema mimi nilifanyika baba kwenu katika Kristo Yesu. 16 Ndiyo sababu ninawahimiza mfuate mfano wangu. 17 Ndiyo sababu ninamtuma Timotheo kwenu. Ni mwanangu katika Bwana. Ninampenda na ni mwaminifu. Atawasaidia ili mkumbuke namna ninavyoishi kama mfuasi wa Kristo Yesu, kama ninavyofundisha katika kila kanisa kila mahali ninakokuwa.
18 Baadhi yenu mnajivuna, mkidhani kuwa sitakuja kuwatembelea tena. 19 Lakini nitakuja kwenu hivi karibuni ikiwa Bwana atanijalia. Ndipo nitajua ikiwa hawa wanaojivuna wana nguvu za kutenda jambo lolote zaidi ya kuzungumza. 20 Mungu huonesha kuwa anatawala katika maisha kwa yale wanayoweza kufanya na si kwa maneno yao. 21 Je, nitakapokuja kwenu, nije nikiwa na adhabu au nije kwa upendo na upole?
© 2017 Bible League International