Revised Common Lectionary (Complementary)
4 Ninalolisema ni hili: Wakati mrithi wa vyote alivyomiliki baba yake bado ni mdogo, hana tofauti yo yote na mtumwa. Haijalishi kuwa anamiliki vitu vyote. 2 Wakati wa utoto bado anapaswa kuwatii wale waliochaguliwa kumtunza. Lakini anapoufikia umri ambao baba yake ameuweka, anakuwa huru. 3 Ndivyo ilivyo hata kwetu sisi. Mwanzoni tulikuwa kama watoto, tukiwa watumwa wa mamlaka za uovu[a] zinazoutawala ulimwengu huu wa sasa. 4 Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu akamtuma Mwanaye, aliyezaliwa na mwanamke na akaishi chini ya sheria. 5 Mungu alifanya hivi ili aweze kuwaweka huru wale waliokuwa chini ya sheria. Kusudi la Mungu lilikuwa kutuasili[b] sisi kama watoto wake.
6 Ninyi sasa ni watoto wa Mungu. Na ndiyo sababu Mungu amemtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu. Huyo Roho aliye ndani yetu hulia “Aba,[c] yaani Baba.” 7 Sasa ninyi si watumwa kama mwanzo. Ni watoto wa Mungu, na mtapokea kila kitu ambacho Mungu aliwaahidi watoto wake. Hii yote ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu amewatendea ninyi.
© 2017 Bible League International