Revised Common Lectionary (Complementary)
Mariamu Amsifu Mungu
46 Mariamu akasema,
“Moyo wangu unamwadhimisha Bwana,
47 kwa maana, Yeye, Mungu na Mwokozi
wangu amenipa furaha kuu!
48 Kwa maana ameonesha kunijali,
mimi mtumishi wake, nisiye kitu.
Na kuanzia sasa watu wote
wataniita mbarikiwa.
49 Kwa kuwa Mwenye Nguvu amenitendea mambo makuu.
Jina lake ni takatifu.
50 Na huwapa rehema zake wale wamchao,
kutoka kizazi hadi kizazi.
51 Ameonesha nguvu ya mkono wake;
Amewatawanya wanaojikweza.
52 Amewaangusha watawala kutoka katika viti vyao vya enzi,
na kuwakweza wanyenyekevu.
53 Amewashibisha wenye njaa kwa mambo mema,
na amewatawanya matajiri bila ya kuwapa kitu.
54 Amemsaidia Israeli, watu aliowachagua ili wamtumikie.
Amekumbuka kuonesha rehema;
55 Maana ndivyo alivyowaahidi baba zetu,
Ibrahimu na wazaliwa wake.”
Uwe Mstahimilivu
7 Hivyo kina kaka na kina dada, muwe na subira; hadi kuja kwa mara ya pili kwa Bwana. Kumbukeni kuwa mkulima huyasubiria mazao yake yenye thamani yakue ardhini. Huyangoja kwa subira mpaka yapate mvua za masika na za vuli.[a] 8 Hata ninyi pia mnapaswa kungoja kwa subira. Muwe imara mioyoni mwenu, kwa sababu kuja kwa Bwana mara ya pili kumekaribia. 9 Kaka na dada zangu, msiendelee kunung'unikiana ninyi kwa ninyi, ili msije kuhukumiwa kuwa na hatia. Tazameni! Hakimu anasimama mlangoni akiwa tayari kuingia ndani.
10 Kina kaka na kina dada, fuateni mfano wa manabii waliosema kwa jina la Bwana. Wao walipata mateso mengi mabaya lakini walivumilia.
2 Yohana alipokuwa gerezani, alisikia kuhusu mambo yaliyokuwa yanatokea; mambo ambayo Masihi angefanya. Hivyo akawatuma baadhi ya wafuasi wake kwa Yesu. 3 Wakamuuliza, “Wewe ni yule tuliyekuwa tunamngojea, au tumsubiri mwingine?”
4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mliyosikia na kuona: 5 Vipofu wanaona. Viwete wanatembea. Watu wenye magonjwa ya ngozi wanaponywa. Wasiyesikia wanasikia. Wafu wanafufuliwa. Na habari njema inahubiriwa kwa maskini. 6 Heri ni kwa wale wasio na shida kunikubali.”
7 Wafuasi wa Yohana walipoondoka, Yesu alianza kuongea na watu kuhusu Yohana. Alisema, “Ninyi watu mlikwenda jangwani kuona nini? Mtu aliye dhaifu, kama unyasi unaoyumbishwa na upepo? 8 Hakika, ni nini mlichotarajia kuona? Aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hivyo. Watu wote wanaovaa mavazi mazuri wanapatikana katika ikulu za wafalme. 9 Hivyo mlitoka kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yeye ni zaidi ya hilo. 10 Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:
‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’(A)
11 Ukweli ni kuwa Yohana Mbatizaji ni mkuu kuliko yeyote aliyewahi kuja katika ulimwengu huu. Lakini hata mtu asiye wa muhimu katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.
© 2017 Bible League International