Revised Common Lectionary (Complementary)
Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu
(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Yh 1:19-28)
3 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, ambapo:
Pontio Pilato alikuwa gavana wa Uyahudi;
Herode alikuwa mtawala wa Galilaya;
Filipo ndugu yake Herode alikuwa mtawala wa Iturea na Trakoniti;
na Lisania, alikuwa mtawala wa Abilene.
2 Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Katika kipindi hiki, Yohana, mwana wa Zakaria, alikuwa akiishi jangwani na alipata ujumbe kutoka kwa Mungu. 3 Alipita katika maeneo yote yaliyo karibu na Mto Yordani akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. 4 Hii ni kama maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya, yanayosema,
“Kuna mtu anayeipaza sauti yake kutokea nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
nyoosheni njia kwa ajili yake.
5 Kila bonde litajazwa,
na kila mlima na kilima vitasawazishwa.
Barabara zilizopinda zitanyooshwa,
na barabara zenye mashimo zitasawazishwa.
6 Na kila mtu ataona
jinsi Mungu atakavyowaokoa watu wake.’”(A)
7 Makundi ya watu walimwendea Yohana ili awabatize. Lakini aliwaambia, “Enyi nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? 8 Badilisheni mioyo yenu! Kisha onesheni ya kuwa mmebadilika kwa namna mnavyoishi. Ninajua mtasema kuwa, ‘Ibrahimu ni baba yetu.’ Hilo halijalishi chochote. Ninawaambia Mungu anaweza kumwumbia Ibrahimu watoto kutokana na mawe haya! 9 Na sasa shoka liko tayari kukata miti,[a] kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”
10 Watu wakamwuliza Yohana, “Tufanye nini?”
11 Akajibu, “Ukiwa na mashati mawili mpe moja asiyekuwa na shati. Kama una chakula, kigawe pia.”
12 Hata watoza ushuru walikuja kwa Yohana. Walitaka wabatizwe. Walimwambia, “Mwalimu, tufanye nini sisi?”
13 Akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi kuliko kiwango kilichoamriwa.”
14 Askari wakamwuliza, “Vipi kuhusu sisi? Tufanye nini?”
Akawaambia, “Msitumie nguvu au kutengeneza mashtaka ya uongo ili watu wawape pesa. Mtosheke na mishahara mnayopata.”
15 Kila mtu alitarajia kuja kwa Masihi,[b] na walijiuliza wakisema, “Labda Yohana ndiye Masihi.”
16 Yohana aliwajibu watu wote, akasema, “Ninawabatiza ninyi katika maji, lakini yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17 Yuko tayari sasa kuja kusafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri na makapi, na kuiweka katika ghala yake kisha ataichoma ile isiyofaa katika moto usiozimika.” 18 Hivi ndivyo ambavyo Yohana aliwahubiri watu Habari Njema. Aliwaonya sana kuwa wanatakiwa kubadili njia zao.
© 2017 Bible League International