Revised Common Lectionary (Complementary)
Kufa kwa Dhambi Lakini Hai Kwa Ajili ya Mungu
6 Hivyo, je, mnadhani inatupasa tuendelee kutenda dhambi ili Mungu atupe neema nyingi zaidi na zaidi? 2 Hapana! Utu wetu wa zamani wa dhambi ulikwisha. Umekufa. Je, tutaendeleaje kuishi katika dhambi? 3 Je, mmesahau kwamba sisi sote tulifanyika sehemu ya Kristo Yesu tulipobatizwa? Katika ubatizo wetu tulishiriki katika kifo chake. 4 Hivyo, tulipobatizwa, tulizikwa pamoja na Kristo na kushiriki katika kifo chake. Na kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa nguvu ya ajabu ya Baba, ndivyo nasi tunaweza kuishi maisha mapya sasa.
5 Kristo alikufa, nasi tumeunganishwa pamoja naye kwa kufa kama yeye alivyokufa. Kwa hiyo tutaunganishwa pamoja naye kwa kufufuka kutoka katika kifo kama yeye alivyofanya. 6 Tunajua kuwa utu wetu wa zamani ulikufa msalabani pamoja naye. Hivyo ndivyo maisha ya utumwa tuliyokuwa nayo yalivyoangamizwa ili tusiendelee kuitumikia dhambi tena. 7 Yeyote aliyekufa amewekwa huru kutoka katika nguvu za dhambi.
8 Ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunajua kwamba tutaishi pamoja naye pia. 9 Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na tunajua kuwa hawezi kufa tena. Sasa mauti haina nguvu juu yake. 10 Ndiyo, Kristo alipokufa, alikufa ili aishinde nguvu ya dhambi mara moja, na siyo mara nyingine tena. Sasa anao uzima mpya, na uzima wake huo upo kwa nguvu za Mungu. 11 Kwa namna hiyo hiyo, mnapaswa kujiona kama mliokufa kwa dhambi na mlio hai kwa nguvu za Mungu kupitia Kristo Yesu.
© 2017 Bible League International