Revised Common Lectionary (Complementary)
11 Nalisema hili kwa sababu mnajua kwamba tunaishi katika wakati ulio muhimu. Ndiyo, ni wakati wenu sasa kuamka kutoka usingizini. Wokovu wetu sasa uko karibu zaidi kuliko ilivyokuwa tulipoamini kwa mara ya kwanza. 12 Usiku karibu umekwisha. Na mchana karibu unaingia. Hivyo tunapaswa kuacha kufanya chochote kinachohusiana na giza. Tunapaswa kujiandaa kuupiga uovu kwa silaha za nuru. 13 Tunapaswa kuishi katika njia sahihi, kama watu walio wa mchana. Hatupaswi kuwa na tafrija za ovyo ama kulewa. Hatupaswi kujihusisha katika dhambi ya uzinzi au ya aina yoyote ya mwenendo usiofaa. Hatupaswi kusababisha mabishano au kuwa na wivu. 14 Bali, muwe kama Kristo Yesu katika kila jambo mnalolitenda,[a] ili watu watakapowaangalia, waweze kumwona yeye. Msifikirie namna ya kuridhisha matakwa ya udhaifu wa mwanadamu na tamaa zake.
Mungu Peke Yake Ndiye Ajuaye Siku ya Kurudi kwa Mwana wa Adamu
(Mk 13:32,35; Lk 17:26-30,34-36)
36 Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua.
37 Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. 38 Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. 39 Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote.
Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. 40 Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42 Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. 43 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. 44 Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia.
© 2017 Bible League International