Revised Common Lectionary (Complementary)
8 Mimi ni Yohana. Mimi ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Baada ya kuyasikia na kuyaona, niliinama chini kusujudu miguuni pa malaika aliyeyaonesha kwangu. 9 Lakini malaika aliniambia, “Usinisujudie mimi! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako manabii, ni mtumishi kama wale wote wanaoyatii maneno yaliyo katika kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
10 Kisha malaika akaniambia, “Usiyafanye siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, wakati umekaribia kwa mambo haya kutokea. 11 Kila atendaye mabaya aendelee kutenda mabaya. Yeyote aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Atendaye mema aendelee kutenda mema. Aliye mtakatifu aendelee kuwa mtakatifu.”
12 “Sikiliza, nakuja upesi! Nakuja na ujira ili kumlipa kila mtu sawa sawa na matendo yake. 13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14 Heri walioosha kanzu zao.[a] Watakuwa na haki ya kula chakula kutoka kwenye mti wa uzima. Wanaweza kuingia katika mji kwa kupitia katika malango yake. 15 Nje ya mji ni kwa ajili wale waishio kama mbwa; wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wapendao kudanganya na kujifanya wema.
16 Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kukuambia mambo hayo kwa ajili ya makanisa. Mimi ni mzao wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi.”
17 Roho Mtakatifu na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Kila asikiaye hili aseme pia, “Njoo!” Wote wenye kiu waje wanywe maji ya uzima bure ikiwa wanataka.
18 Ninamwonya kila mtu anayesikia maneno ya unabii wa kitabu hiki: Ikiwa mtu yeyote ataongeza chochote kwa haya, Mungu atampa mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19 Na ikiwa mtu yeyote akitoa sehemu yoyote ya maneno ya kitabu hiki cha unabii, Mungu ataondoa sehemu ya urithi wa mtu huyo katika mti wa uzima na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yesu ndiye anayesema kwamba haya yote ni kweli. Sasa anasema, “Ndiyo, naja upesi.”
Amina! Njoo, Bwana Yesu!
21 Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja na watu wote.
© 2017 Bible League International