Revised Common Lectionary (Complementary)
Utumieni Uhuru Wenu Kumtukuza Mungu
23 Mnasema “Vitu vyote vimeruhusiwa.” Lakini si vitu vyote vinafaa. “Vitu vyote vimeruhusiwa.” Lakini vitu vingine havisaidii katika kuliimarisha kanisa. 24 Jitahidi kuwafanyia mema wengine badala ya kufanya mema kwa ajili yako wewe wenyewe.
25 Kuleni chakula chochote kinachouzwa sokoni. Msiulize maswali ili kutafuta kujua kama ni sahihi ama la kwako kukila. 26 Mnaweza kula chakula hicho, “Kwa sababu dunia na kila kitu kilichomo ndani yake ni vya Bwana.”(A)
27 Asiye mwamini anaweza kuwaalika kula chakula. Ikiwa mtakwenda, basi mle chochote kitakachowekwa mbele yenu. Msiulize ulize maswali. 28 Lakini mtu akiwaambia, “Chakula hicho kilitolewa sadaka katika hekalu la miungu,” basi msile. Kwa sababu kinaweza kumwathiri mtu na uhusiano wake na Mungu. 29 Na hapa sizungumzii kuhusu uhusiano wenu na Mungu, bali uhusiano wa mtu yule aliyewaambia na Mungu. Kwa nini uhuru wangu mwenyewe uhukumiwe na mawazo ya mtu mwingine? 30 Ikiwa mimi nitakula chakula nikiwa na shukrani, kwa nini basi nisikosolewa kwa sababu ya kitu ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?
31 Ninachosema ni kwamba: ukila, au ukinywa, au ukifanya jambo lolote, lifanye kwa ajili ya utukufu wa Mungu. 32 Kamwe usifanye jambo lolote litakalowafanya watu wengine kutenda mabaya, iwe ni Wayahudi, wasio Wayahudi au mtu yeyote katika kanisa la Mungu. 33 Ninafanya vivyo hivyo. Ninajitahidi kwa njia yeyote ile kumpendeza kila mtu. Mimi sijaribu kutenda yaliyo mema kwangu. Ninajaribu kutenda yale yaliyo na manufaa kwa watu wengine ili waweze kuokoka.
11 Fuateni mfano wangu, kama ninavyoufuata mfano wa Kristo.
© 2017 Bible League International